MNH walalamikia kukosa mishahara

Wafanyakazi wapya katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili(MNH), wamelalamikia kutolipwa mishahara kwa miezi minne sasa, huku uongozi ukishindwa kuwapa majibu ya ufumbuzi wa tatizo hilo.
Wafanyakazi hao zaidi ya 50 walioajiriwa tangu mwezi wa nane mwaka huu, waliliambia gazeti hili kwa nyakati tofauti kuwa hawajalipwa hata shilingi moja tangu walipoajiriwa.
Walilalama kwamba kilichofanyika hadi sasa ni baadhi yao kupewa namba za hundi, lakini walipokwenda kuangalia kwenye akaunti zao hawakukuta kitu.
“Sisi tunashangaa kukaa muda wote huu bila kulipwa hata senti tano, huku tukipangiwa majukumu. Kama tumeajiriwa na Serikali, si inakuwa imeshatenga bajeti yetu kabisa, kwa nini tunapata usumbufu huu? Haki ipo wapi? ” alilalama mmoja wa wafanyakazi hao wanaofanya kazi idara mbalimbali wakiwamo wauguzi, watunza kumbukumbu na masijala.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano cha Hospitali hiyo, Aminiel Aligaesha alikiri kuwapo kwa hali hiyo.
Hata hivyo alisema wafanyakazi wenye madai hayo ni 10 na wataanza kulipwa mwisho wa mwezi huu. “Ni kweli hawajalipwa mishahara tangu walipoajiriwa Agosti mwaka huu kwa sababu majina yao yalikuwa hayajaingizwa kwenye utaratibu wa malipo wa Serikali,”alisema.

Post a Comment

Previous Post Next Post