KAMA sinema vile! Simba wamempandisha ndege na kumleta Dar es
Salaam kiraka wa Mbeya City, Deus Kaseke na kumhifadhi kwenye hoteli
moja maeneo ya Ubungo, Dar es Salaam, lakini Yanga walikuwa kimya
wanafuatilia mchongo wote unavyokwenda.
Kuanzia Simba ilipomweka, dau wanalotaka kumpa na
mshahara wanaopanga kumlipa kisha wakatafuta upenyo wakamvaa mchezaji
huyo hotelini bila Simba kujua.
Yanga walitua kwenye hoteli hiyo na kumshawishi
kisha kufanikiwa kumwondoa hapo na kumpeleka eneo jingine kabisa kufanya
naye mazungumzo kwa lengo la kuipiga bao Simba, lakini wakakwama kwenye
mambo kadhaa.
Yanga walimuahidi dau mchezaji huyo na kutaka
kumuondoa kabisa kwenye hoteli ambayo alikuwa amepangishiwa na Simba
wakamlaze sehemu nyingine wakati wanamalizana nae lakini Kaseke akakomaa
akitaka kumalizana na Simba kistaarabu lakini vilevile akiisisitiza
Yanga iweke fungu la maana mezani.
Ilikuwa hivi; Ndani ya saa 48 viongozi wa Simba
na Yanga walijaribu kuzidiana akili kuhakikisha wanampata Kaseke ambaye
bado ana mkataba wa miezi sita na timu yake inayosuasua kwenye Ligi Kuu
Bara.
Vigogo wa juu wa Simba walizungumza na mchezaji
huyo na kumuahidi kwamba watampa Sh20 milioni asaini mkataba wa miaka
miwili, lakini walimwambia kwamba watampa nusu kwanza ili Desemba Mosi
asaini halafu mapema mwakani amaliziwe kilichobaki naye akagoma kwa
madai kuwa dau hilo ni dogo na anataka alipwe chake chote. Mchezaji huyo
aliwakomalia Simba akitaka waongeze fedha kufikia Sh40 milioni ndipo
asaini lakini vigogo hao nao wakamkomalia.
Baadaye Yanga wakamtafuta na kumpata kisha
wakamfungia chumbani katika hoteli nyingine kwa mazungumzo ambapo
wenyewe walifika dau la Sh22 milioni kwa vile tayari walishasikia kwamba
Simba wanampa Sh20 milioni.
Habari za uhakika zinadai kwamba Simba walimpa
mkataba akausome kisha awajibu lakini baadaye Yanga wakamtumia mtoto wa
kigogo maarufu nchini ambaye ni mnazi wa Yanga kumlainisha Kaseke
ikashindikana.
Yanga walimuahidi mchezaji huyo kiasi hicho cha
fedha lakini mkononi aliyekuwa akimshawishi alikuwa na milioni moja tu,
mchezaji huyo alivyoonyesha kwamba hana dalili ya kulainika akapigiwa
simu kiongozi mmoja wa Mbeya City amshawishi lakini bosi huyo akadai
kwamba hayo ni mambo binafsi hawezi kuingilia.
Habari ambazo Mwanaspoti ilizipata jana Alhamisi
jioni kutoka Mbeya City ni kwamba wamemuongezea mshahara hadi Sh900,000
ili asiondoke na sasa anakuwa ndiye mchezaji anayelipwa ghali zaidi
kwenye kikosi hicho kuanzia mwezi huu.
Licha ya kugoma kutoa ushirikiano katika sakata
lake, Mwanaspoti linaweza kuthibitisha kwamba mchezaji huyo yupo Dar es
Salaam na ataondoka kurudi Mbeya leo Ijumaa au kesho Jumamosi.
“Nipo Dar es Salaam kwa mambo yangu binafsi na
Jumanne nitajiunga na timu yangu kambini Mbeya, kuhusu habari za Simba
na Yanga ukifika muda nitakueleza vizuri lakini sasa nawaza Mbeya City.”
alisema.
- MwanaSpot
- MwanaSpot
Post a Comment