Zimamoto: Sababu zinazotukwamisha hizi hapa

Kikosi cha zimamoto
Jeshi la  Zima Moto na Uokoaji limesema kuwa ukosefu wa vitendea kazi, rasilimali watu pamoja na ufinyu wa fedha wanazokusanya kutoka kwa wananchi, ni changamoto zinazokwamisha Jeshi hilo kushindwa kutoa  huduma za uhakika kwa jamiii pindi majanga ya moto yanapotokea.

Akizungumza na NIPASHE, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa  Umma  wa Jeshi hilo,  Miraji  Killo alisema:

“Tunapokea malalamiko mengi sana kutoka kwa wananchi kutokana na kutoridhishwa na huduma zetu, lakini sisi tumejipanga kumaliza changamoto zote na kutoa huduma bora kwa jamii hasa katika majanga ya moto.”

Alisema kuwa magari makubwa ya  kuzimia moto yaliyopo hivi sasa hayaendani na mabadiliko ya kukua kwa miji nchini kutokana na hivi sasa maghorofa marefu yanayojengwa na Jeshi hilo hayana vifaa vya kisasa vya kuzimia moto.

“Zamani tulikuwa tukienda kwenye tukio hatuishiwi na maji kutokana  na visima vyetu kuwa na maji ya kutosha tofauti na sasa, kuna shida kubwa ya maji, visima vingi vimefukiwa kutokana na ujenzi  wa  barabara,”  alisema Killo.

Alisema Jeshi hilo limefanya mazungumzo na wenyeviti wa serikali za mitaa wote kujenga visima vya maji katika mitaa yao ili janga lolote la moto likitokea wapate huduma kwa haraka.

Zimamoto wamekuwa wakilalamikiwa na kila uchao na wananchi kutokana na kuchelewa kufika maeneo ya majanga na wakati mwingine wanapoishiwa na maji wanashindwa kupata mengine na matokeo yake ni majengo na mali nyingine kuteketea.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post