Dodoma/Dar. Siku moja kabla ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC) kuwasilisha bungeni, ripoti ya uchunguzi wa IPTL kuhusu
ufisadi katika akaunti ya Escrow, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Zitto Kabwe
amesema amekuwa akipata vitisho ili kuzuia ripoti hiyo.
Akizungumza jana, Zitto alisema pamoja na vitisho hivyo haogopi kwa kuwa maisha yake ameshayaweka nadhiri siku nyingi.
“Kuna kundi la wahuni kutoka Musoma limeletwa
Dodoma likiongozwa na mtu (jina tunalihifadhi) mwenye rekodi ya
ujambazi. Hivi sasa anashikiliwa na polisi kwa kukutwa na nyaraka
zilizoibwa Ofisi ya Bunge. Usalama wa wajumbe wote wa PAC upo shakani,”
alisema Zitto.
Aliongeza kuwa kuna vipeperushi vimesambazwa mjini
Dodoma kumkashifu lakini havitamsumbua kwa kuwa yeye anataka ukweli
ujulikane.
Baadhi ya wabunge jana walionekana na kitabu
kilichoandikwa ‘mjue Zitto Kabwe kama mtetezi wa wanyonge,’ lakini ndani
yake kikiwa na mambo ya kumchafua mbunge huyo.
Vitabu hivyo vinaelezwa kusambazwa kwa wabunge
katika nyumba zao vikilenga kuonyesha kwamba Zitto hafai kusimamia PAC
ambayo hivi sasa inashughulikia escrow.
Wakati Zitto akisema hayo, suala hilo la vitisho
jana pia liliibuka bungeni baada ya Mbunge wa Ole (CUF), Rajab Mbarouk
Mohamed kueleza kuwa hali ni tete kuhusu usalama wa wabunge kutokana na
escrow.
Akiuliza swali la nyongeza, Mohamed alisema
usalama wa wabunge uko shakani kuanzia maeneo wanayofanyia kazi na
makazi yao na hasa kipindi hiki tangu kuanza kwa sakata la escrow.
“Je, nini tamko la Serikali juu ya ulinzi na
usalama wa wabunge katika maeneo ya kazi, pia katika maeneo yao ambayo
wanaishi?” alihoji.
Kabla ya majibu kutolewa na Serikali, Spika wa
Bunge, Anne Makinda ambaye jana alianza kuongoza vikao baada ya safari
yake nje ya nchi, aliingilia kati akisema ofisi yake inakusudia kujenga
kijiji cha wabunge ambako watalindwa kwa pamoja.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba alisema Serikali inafanya
tathmini ya vitisho vyote vya viongozi nchini wakiwamo wabunge ili
kuhakikisha wanakuwa salama.
- Soma Zaidi Hapa(Mwananchi)
- Soma Zaidi Hapa(Mwananchi)
Post a Comment