Ahimiza elimu ya umiliki wa ardhi kwa madiwani

Chemba. Katibu Tawala wa Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma, Dorah Makinga amelitaka Jumuiko la Maliasili Tanzania (TNRF), kuwaelimisha madiwani matumizi bora ya ardhi ili wakawaelimisha wananchi katika ngazi za vijiji na vitongoji.
Makinga aliyasema hayo katika warsha ya kuzungumzia matumizi bora ya ardhi sambamba na kupatiwa ripoti ya utafiti uliofanywa na TNRF katika Tarafa ya Kwamtoro wilayani hapa. Alisema migogoro ya ardhi imekuwa chanzo cha kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi.
“Nawaomba mpange bajeti ya kuwezesha kufanya mafunzo kwa viongozi wetu kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji na wilaya ili wajue nini chakufanya wanapokutana na migogoro ya ardhi kwenye maeneo yao.
Mratibu TNRF, Godfey Massay alikiri kuwapo kwa migogoro mingi ya ardhi katika tarafa hiyo kutokana na utafiti uliofanyika na kutoa wito kwa viongozi wa Serikali na wale wa siasa kutoa ushirikiano ili kuitatua.
“Hii ni hatua ya mwanzo katika mradi huu wa ardhi, tumefanya utafiti wa mwanzo na kugundua Tarafa ya Kwamtoro inakabiliwa na changamoto nyingi katika ardhi, ikiwamo ya ardhi kutopimwa, hakuna mipango ya matumizi ya ardhi, wakazi wengi hawana hati hata ya kimila ya kumiliki ardhi,” alisema Massay.
Alisema licha ya changamoto hizo, bado eneo hilo hukumbwa na uvamizi wa wageni wanaoingia na kujenga makazi bila kufuata utaratibu.
Diwani wa Kata ya Farkwa, Selemani Gaawa alisema: “Ni bahati kubwa nyie kutufikia katika kipindi hiki kutokana na hali halisi iliyoko katika maeneo mengi ya tarafa hizi.
Ni juzi tu tumetoka kupambana na wahamiaji ambao walisababisha baadhi ya wenyeji hapa kupoteza maisha kutokana na kugombea ardhi.”
- Mwananchi

Post a Comment

أحدث أقدم