AKIMBIWA NA MUME KWA KUZAA MLEMAVU

Stori: MAYASA MARIWATA DUNIA HAINA HURUMA! Mwanamama mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Sarah Lyimo,  mkazi wa Buza Mwang’ati jijini Dar es Salaam amejikuta kwenye wakati mgumu baada ya mumewe aitwaye  Mohammedi kumkimbia baada ya kile alichodai kuwa na mtoto mwenye ulemavu.


Sarah Lyimo akiwa na watoto wake.
Akizungumza na mwandishi wetu wiki iliyopita  kuelezea mkasa mzima wa kutelekezwa  kwake, Sarah alidai aliishi na mwanaume huyo ambaye ni dereva wa bodaboda kwa miaka minne na kufanikiwa kuzaa naye watoto wawili hapa Dar.
Akifafanua zaidi Sarah alisema:  “Mwanzoni  tulipendana sana na mume wangu. Mtoto huyu nilipomzaa alikuwa hana tatizo lolote, alianza kukumbwa na matatizo kwa kuumwaumwa akiwa na miezi sita ndipo akaanza kubadilika na kupatwa na ulemavu wa miguu na mikono.
“Eti ndugu wa mume wanasema kwa kuwa tumempa jina la marehemu babu yake bila ridhaa ya bibi yake ambaye yupo hai ndiyo maana mtoto amelemaa, wakaniambia inabidi twende kaburini tukamuombe radhi (babu yake) ndipo mtoto atapona. Mimi sina imani hizo.

Sarah Lyimo akiwa na mtoto wake aliyepata ulemavu.
“Balaa lilizidi siku hadi siku kwa baba yake kutomjali mtoto huyo kwa matunzo yoyote na kunikashifu akidai eti mtoto wake hawezi kuwa kilema, hata hivyo tulikuwa tukiishi kwa tabu nikapata mimba na  mwanzoni mwa mwaka jana nikaenda kujifungulia kijijini kwetu Moshi, niliporudi nikakuta anaishi na mwanamke mwingine, ndipo aliponiacha na sasa nimebaki nahangaika, pa kuishi sina naishi na wanangu kwa marafiki, amenitelekeza.”  
Alisema kutokana na ugumu wa maisha alionao anadhani bora arudi kwao Moshi, kuliko kuendelea kuteseka kwenye jiji asilolifahamu vizuri.

Sarah Lyimo akisikitikia uonevu aliofanyiwa na mume wake, Mohammedi.
“Nawaomba Watanzania wanichangie fedha ya nauli ya kurudi kwetu pia waniwezeshe mtaji ili nikaanzishe mradi wa kujikimu kimaisha na wanangu,” alisema Sarah.Wakati Uwazi linakwenda mitamboni, Sarah alisema mtoto huyo amefariki dunia Ijumaa iliyopita.

Post a Comment

Previous Post Next Post