CCM kutumia panga la 2005

Dar es Salaam. Vigezo 13 vilivyowekwa na CCM katika Uchaguzi Mkuu wa 2005 kumpima mwanachama anayefaa kugombea urais, ndivyo vitakavyotumika kuwaengua makada wanaoendelea kujitokeza kuwania nafasi hiyo mwakani, imefahamika.
Vigezo hivyo vinaonekana kuwa kizingiti kwa baadhi ya makada wa chama hicho ambao tayari wametangaza na wengine wanaotajwa kutaka nafasi hiyo ya juu nchini, ukiachilia mbali mnyukano unaotarajiwa kutoka vyama vya upinzani vinavyoonekana kupata nguvu.
Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula amelithibitishia gazeti hili kwamba, “Sifa hizo 13 zilizotumika mwaka 2005 na 2010 ndizo zitakazotumika pia mwaka 2015 na wala hakutakuwa na maboresho wala nyongeza ya aina yoyote.”
Vigezo hivyo viliwekwa ili kuhakikisha chama hicho kinampata mgombea asiyetiliwa shaka juu ya vitendo vya uadilifu, mwenye uzoefu wa uongozi serikalini, atakayedumisha muungano, mwenye upeo wa masuala ya kimataifa, mtetezi wa wanyonge, asiyejilimbikizia mali na mwajibikaji, mambo ambayo hata hivyo, bado yameibua mjadala iwapo yanazingatiwa au la.
Pia anayetakiwa lazima awe mwenye kuzitetea sera za CCM, anayekubalika na wananchi, asiye na hulka ya udikteta au ufashisti, mwenye uwezo wa kufanya uamuzi wa busara na kiwango cha elimu ya chuo kikuu au inayolingana nayo.
Licha ya vigezo hivyo, baadhi ya makada waliokwishajitokeza na wengine wanaotajwa wanaonekana dhahiri kukosa baadhi sifa hizo na wengine wako ‘kifungoni’ kwa miezi 12 baada ya kupewa onyo kali kwa kufanya kampeni mapema na kujihusisha na vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya chama na jamii.
Vigogo wa CCM ambao wanatajwa kutaka kupewa ridhaa ya kupeperusha bendera ya chama hicho ambao iwapo watachukua fomu, watatazamwa kwa vigezo hivyo ni Mbunge wa Nzega, Dk Khamis Kigwangalla, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba ambao wamekwishatangaza kuwania nafasi hiyo.
Wengine ambao wanatajwa ingawa hawajatangaza nia hadharani ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa; Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa; Bernard Membe; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu); Stephen Wasira na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
Wachambuzi wanavyosema
Akizungumzia vigezo hivyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini, Danford Kitwana alisema CCM inajua kuwa hakuna mgombea anayeweza kuwa na sifa zote 13, kwa hiyo inapaswa iangalie ni nani anawazidi wengine.
“Kigezo cha kuwa na sifa ya maadili ndicho kinachowakwamisha wengi, pia hakuna mgombea anayeweza kuwa na sifa zote zilizowekwa na chama, mwingine anaweza kuwa na sifa saba, nne au tano.
“Wakitumia mfumo wa kuwatazama wagombea wao kwa idadi ya sifa, mtu mwenye sifa nyingi ndiye asimamishwe kugombea.”
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post