KATIBA MPYA : Kura tatu zawaweka njiapanda Wazanzibari

Wananchi wa Zanzibar wapo katika matayarisho ya kupiga kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa baada ya Bunge la Katiba kukamilisha majukumu yake Oktoba mwaka huu na kubakia kura ya maoni mwakani.

Upingaji wa kura utatanguliwa na elimu ya uraia ambayo itatolewa na kamati maalumu ambazo zitaundwa kwa ajili ya kufanikisha kazi hiyo mbali na makundi ya wanaharakani na vyama vya siasa.

Kama Katiba hiyo itafanikiwa kupita, Tanzania itakuwa imeandika historia mpya baada ya miaka 50 kuandika Katiba inayotokana na ushirikishwaji wa wananchi wa pande mbili za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Maneno mawili yametawala sana katika mijadala Zanzibar hasa katika mabaraza ya kahawa na masikani watu kwa makundi ya vijana, wazee na wanasiasa wakitumia muda mwingi kubishana kama Katiba Inayopendekezwa itapita au.

Matokeo ya kura ya maoni yanasubiriwa kwa hamu kwa sababu ndiyo dira ya kutoa mwelekeo wa Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwakani.

Makundi yaibuka

Tayari kumeibuka makundi matatu Zanzibar, kila moja likiwa na mtazamo wake kuhusu kura ya maoni.

Wapo wanaofanya kampeni ya kutaka kuungwa mkono kwa maana ya kupigiwa kura ya ndio, wengine wanaendesha kampeni ya kutaka wananchi wapige kura ya hapana, lakini kundi la tatu linalofanya kampeni ya kuwataka wananchi kususia zoezi zima la kura ya maoni itakayofanyika mwakani.

Kususia kura

Waziri wa zamani wa SMZ, Mansoor Yusuph Himid amekuwa mwanasiasa wa kwanza kujitokeza hadharani na kuwataka Wazanzibari kususia kura ya maoni kwa madai Katiba Inayopendekezwa ni kitanzi kipya kwa Zanzibar kiuchumi na kisiasa.

Anasema kwamba kitendo cha Wazanzibari kushiriki kura hiyo ni sawa na mtu kushiriki kula chakula ambacho hakushiriki kupanga bajeti, kupika au kupakua.

Mansoor, aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya CCM na SMZ, anakwenda mbali zaidi kwa kusema kama Katiba hiyo itapitishwa, Zanzibar itaendelea kubanwa katika kujiamulia mambo yake ya kiuchumi na kisiasa.
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post