Phiri bye bye Simba


ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa timu ya Simba, Mzambia Patrick Phiri, amesema alikuwa anajua hatima ya kibarua chake ni kuondolewa, hivyo hana kinyongo na uongozi wa klabu ya Simba.
Akizungumza na Jambo Leo, Dar es Salaam jana, Phiri alisema alijua nini hatima yake hivyo, kwa matokeo ya timu yake hana kinyongo na kiongozi yoyote wa timu hiyo.
Phiri aliwasili nchini Agosti 13 mwaka huu na kuingia mkataba wa mwaka mmoja na Simba, akichukua nafasi ya kocha kutoka Serbia, Zdravko Logarusic ambaye mkataba wake wa mwaka mmoja ulivunjwa, baada ya awali kumaliza mkataba wa miezi sita katika klabu hiyo, aliyechukua nafasi ya Abdallah Kibaden.
Uongozi wa Simba uliamua kuvunja mkataba wa Phiri usiku wa kuamkia jana kutokana na kutoridhishwa na matokeo iliyopata katika Ligi Kuu ya Vodacom inayoendelea ambapo kati ya mechi nane, imeshinda mchezo mmoja imefungwa mmoja na kutoka sare mechi sita, ina pointi tisa.
Kwa matokeo hayo, Simba imepoteza pointi 15 katika michezo nane pointi (12 kwa kutoka sare mechi sita na pointi tatu kwa kufungwa dhidi ya Kagera Sugar).

Phiri alisema jana kuwa siku zote anatambua uwepo wa kocha kwenye timu unategemea kufanya vizuri, inapofanya vibaya huwa ni kinyume chake yaani huondolewa.
Alisema yeye kama kocha hajapenda timu ifanye vibaya, lakini matokeo ya mechi zake zimefanya aondolewe.
“Sio Simba tu hata timu nyingine yoyote inahitaji matokeo mazuri, hivyo kuondolewa kwangu kuifundisha Simba ni kitu kinachoeleweka, hata mimi sijapenda timu ifanye vibaya lakini ndiyo hivyo,” alisema.
Phiri alisema anatarajia kuondoka nchini ndani ya siku mbili, baada ya kumalizana na uongozi wa klabu hiyo, anasubiri kulipwa haki zake baada ya kusitisha mkataba wake.
Pamoja na kusitishwa mkataba, kocha huyo jana aliungana na wachezaji wake katika mazoezi ya timu hiyo, yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Sigara, Dar es Salaam pengine ikiwa ni kwa lengo la kuwaaga rasmi.
Phiri alionekana akiwa wa kawaida, wala hakuonesha kuwa mnyonge, kama inavyokuwa kwa makocha wengine.
Aliwasili Agosti 13 mwaka huu na kulakiwa kwa shangwe na mashabiki wakiwa na matumaini kuwa angeifanya ipate mafanikio kama ilivyokuwa msimu wa 2009/10 ambapo iliipatia ubingwa.
Akizungumza wakati huo Phiri alisema : “Nimerudi tena Simba kurejesha heshima na mafanikio yaliyopotea,” alisema.
Nafasi ya Phiri, inachukuliwa na Goran Kopunovic raia wa Serbia, ambaye anatarajiwa kuwasili leo na kuingia mkataba wa mwaka mmoja kuinoa timu hiyo.
Kuponovic aliwahi kuinoa Polisi Rwanda kwa mafanikio makubwa na kuiwezesha kuwa tishio mbele ya vigogo APR na Rayon.

Post a Comment

Previous Post Next Post