Mwakyembe kuwaweka kiti moto vigogo TICTS

Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe.
Kikao baina ya Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe na wadau wa bandari ya Dar es Salaam, kimeibua ufisadi unaodaiwa kufanywa na Kampuni ya Kupakua na Kupakia Kontena Bandarini (TICTS), ambao umekuwa ukiwaumiza wateja wanaotumia bandari hiyo.
Ufisadi huo, ambao uliibuliwa katika kikao hicho jana na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wakala wa Forodha na Uondoshaji wa Shehena Tanzania (Taffa), Edward Urio, unadaiwa kufanywa na Ticts kwa kuwatoza wateja wa bandari hiyo viwango vya kubadilisha dola ya Marekani kwenda shilingi ya Kitanzania, kinyume cha taratibu za nchi.

Waziri Mwakyembe amemuagiza mtendaji mkuu wa Ticts pamoja na menejimenti yake yote kwenda ofisini kwake leo asaubuhi wakiwa na maelezo ya kutosha kwanini wamekuwa wakikiuka taratibu za nchi na wameanza lini kufanya hivyo.

Kabla ya Waziri Mwakyembe kutoa agizo hilo kwa menejimenti ya Ticts, alitaka kujua kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) kama wana taarifa kuhusiana na kashfa hiyo.

Meneja wa Shughuli za Bandari wa Sumatra, Julius Mtinje, alithibitisha kuwa wanazo na kwamba, wamekwisha kuiadikia Ticts barua kuhusiana na suala hilo.

Meneja wa Titcs, Donald Talawa, alithibitisha kupokea barua hiyo ya Ticts.

Waziri Mwakyembe alisema iwapo mtendaji mkuu wa Ticts na menejimenti yake hawatafika leo ofisini kwakea atamchukulia hatua.

Alisema upo utaratibu wa kisheria wa muda mrefu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) unaotumika kila wiki wa kutoa mwongozo wa viwango vya kubadilisha fedha hizo na kwamba, kila mtu anawajibika kufuata viwango hivyo.

Waziri Mwakyembe alisema ameshtuka kusikia Ticts wana viwango vyao na kusema jambo kamwe hawawezi kulikubali.

“Na ndiyo maana nimesema namtaka mtendaji mkuu wa Ticts kesho (leo) asubuhi saa 2 awe ofisini, kama hajafika kesho saa 2 asubuhi mimi namchukulia hatua. Sisi ni serikali, hatuwezi kuwa tunafanya mzaha mzaha tu. Benki Kuu ya Tanzania yenyewe ndiyo ina-set viwango, na kila mtu lazima aheshimu hivyo. Sasa kila mtu hawezi kuwa na ka-republic kake ana-set ya kwake. Hiyo hatuwezi kukubali,” alisema Waziri Mwakyembe.

Aliongeza: “Na tunajua ana-set viwango ambavyo vinawaumiza sana wateja wa bandari ya Dar es Salaam. Na sisi lengo letu kubwa ni kujenga au kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara wote wanaotaka kutumia bandari yetu ya Dar es Salaam.”

Alionya kuwa iwapo Ticts wataendelea na kashfa hiyo watawachukulia hatua kali.

Katika hatua nyingine, Waziri Mwakyembe, ameipa wiki mbili kampuni ya Ami inayoendesha bandari kavu kumlipa mara moja mtu, ambaye kontena lake lilipotea mikononi mwao, vinginevyo atawafungia kuendelea na shughuli hizo katika bandarini.

Rais wa Chama cha Wafanyabiashara wa Kongo, Mukendi Kabobu, aliwasilisha malalamiko kwa Waziri Mwakyembe, akisema siku 30 walizopewa za kurudisha kontena jijini Dar es Salaam kutoka DRC zimekuwa zikiwabana kwa kuwa ni chache.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post