Sakata la Escrow, Jopo la Majaji kusikiliza zuio la IPTL



Grace Gurisha
JOPO la majaji watatu wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wanatarajia kusikiliza kesi ya Kikatiba iliyofunguliwa na Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL).
Ambayo imeomba zuio la muda la utekelezaji wa maazimio nane ya Bunge kuhusu sakata la Akaunti ya Escrow, baada ya upande wa Serikali kujipanga kujibu hoja za IPTL.
IPTL imefungua kesi hiyo namba 59 ya mwaka huu na Kampuni ya Pan African Power Solutions (T) Limited (PAP) na Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni hizo, Harbinder Sigh Seth wakiomba mahakama kuzuia maazimio husika, ambapo kesi hiyo inaanza kusikilizwa leo.
Jopo hilo ni Augustine Mwarija (Mwenyekiti wa jopo), Jaji Gadi Mjemas na Jaji Stela Mugasha, awali upande wa Serikali uliomba ahirisho ili wajiandae kujibu hoja za zuio hilo, kwa sababu walichelewa kupewa nakala za hoja za zuio za upande wa utetezi.
Ombi la ahirisho hilo liliombwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju aliomba kesi hiyo iahirishwe hadi Desemba 31, mwaka huu kwa sababu walichelewa kupata maombi hayo, kwa hiyo walishindwa kuyasoma kwa muda huo na kuyajibu.
Kampuni hiyo inaomba mahakama izuie utekelezaji wa maazimio ya Bunge yaliyofikiwa Novemba 29, mwaka huu na uamuzi wa Spika wa kuyakubali, kwani ni kinyume cha Katiba.
Katika hati hiyo ya kikatiba wadai hao wanapinga maazimio ya Bunge kutekelezwa wakidai kwamba, kilichofanyika bungeni ni kinyume cha Katiba.
IPTL, PAP na Harbinder Sigh Seth wanadai kwamba, maazimio hayo yanalenga kugombanisha mihimili mitatu ya dola na kwamba, yaliegemea upande mmoja.
Wadai hao wanasisitiza katika hati hiyo kuwa, kuna kesi mbalimbali zinazoendelea mahakamani zinazohusiana na sakata la fedha za Escrow.
Kutokana na sakata hilo, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), walifanya uchunguzi na baadaye taarifa ya CAG ikajadiliwa bungeni na kufikiwa kwa maazimio nane.
Inadaiwa mjadala huo ulisababisha Bunge kufikia maazimio hayo, kitendo ambacho kilipuuza amri ya Mahakama Kuu na kufuata tafsiri potofu iliyotolewa na Waziri wa Katiba na Sheria kuhusu amri iliyozuia mjadala wa Escrow bungeni.
Wadai hao walifungua kesi hiyo dhidi ya Waziri Mkuu, Takukuru, Spika wa Bunge na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG). Kampuni hizo zinawakilishwa na kampuni za uwakili za Bulwark Associates Advocates iliyopo Mikocheni B, Asyla Attorneys iliyopo katika jengo la Alpha House na Marando, Mnyele & Co. Advocates.

Post a Comment

Previous Post Next Post