Dar es Salaam. Viongozi wa CCM, Tawi la Kwembe
wilayani Kinondoni wanadaiwa kuvamia eneo la mjane na kung’oa nguzo za
mpaka wa eneo lake pamoja na kukatakata miti.
Mjane huyo, Aurelia Msuya, ambaye mumewe alifariki
miaka 40 iliyopita, anadai kuwa ameishi hapo tangu mwaka 1987 akiwa
mwalimu wa Shule ya Msingi ya Kwembe.
Akizungumzia tukio hilo, Aurelia anadai kuwa ana
siku tatu hajatoka nje akihofia usalama wake kutokana na vitisho
anavyopata kutoka kwa viongozi hao wa CCM .
Gazeti hili lilishuhudia greda la Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ) likifanya kazi ya kusawazisha eneo la wazi
lililo karibu na nyumba ya mjane huyo ambalo miaka yote limekuwa
likitumiwa na vijana kuchezea mpira.
Naye jirani wa mama huyo, Shadi Yohana alisema:
“Mimi nina mwaka wa saba naishi hapa, ninachoelewa eneo hili
linamilikiwa na huyu mama. “Hawa viongozi wa CCM wote wamemkuta huyu
mama, wanachofanya hapa ni ulafi wa ardhi na hii inatokana na mmoja wa
wastaafu wa jeshi anayetaka kugombea udiwani, nadhani ndiye aliyeleta
haya magari ya jeshi yaje kufanya usafi.”
Mwananchi ilipomtafuta mwenyekiti wa CCM Kwembe,
Said Khalifa alisema, “Huyo mama amejenga kwenye eneo la wazi, anatakiwa
aondoke.
“Hili ni eneo la kijiji na CCM ni wadhamini. Tangu
mwaka 1976 eneo hili lilikuwa likitumiwa na jeshi kwa ajili ya kulenga
shabaha, ndio maana tumewaambia watusaidie kuusawazisha huu uwanja huu,”
alisema mwenyekiti huyo wa CCM.
“Akiendelea kutuchezea tutavunja nyumba au tutamfungia njia tuliyompa ya kupita kwenda kwake, akose pa kupita,” aliongeza.
Naye mwenyekiti wa serikali ya Mtaa wa Kwembe, Idd
Mnyeke alisema: “Mimi hapa ni mgeni, lakini wakati nakabidhiwa ofisi na
mwenyekiti alinikabidhi maeneo mawili ambayo alisema ni mali ya
Serikali, moja ni uwanja wa michezo na eneo la soko, lakini uwanja huo
ambao unaleta mgogoro sikukabidhiwa na sijui lolote.”
Msemaji wa JWTZ, Joseph Masanja alipoulizwa kuhusu
magari ya jeshi kufanya kazi katika eneo hilo, alisema hana taarifa
nayo. “Na hakuna ratiba yoyote inayoonyesha kuwa kuna magari ya jeshi
yanayoendelea na kazi katika maeneo ya Kwembe,” alisema.
- Mwananchi
- Mwananchi
Post a Comment