Chadema chadai kunasa ujumbe wa Rugemalira kwenda kwa JK

Katibu Mkuu wa chama Cha Demokrasia na Maendeleo, Dk. Wilbroad Slaa.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimedai kimenasa ujumbe mwingine wa barua pepe ulioandikwa na mmiliki wa Kampuni ya VIP Engeering, James Rugemalira, kwenda kwa Rais Jakaya Kikwete ukimtaka asitekeleze maazimio yaliyofikiwa na Bunge kuhusu akaunti ya Tegeta Escrow, mpaka uamuzi wa mahakama utakapotolewa.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Wilbroad Slaa, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema barua pepe hiyo iliyoandikwa Desemba mosi, ni mfululizo wa zile alizoandika Novemba 29, mwaka huu, zinazoanza kwa kumtaja ‘Dear JK’  kumweleza kuwa, ameshangazwa na maamuzi ya Bunge na maswali 21 kuhoji mhimili huo.

Alisema siku hiyo ya Novemba 29, alimwandikia kuomba amsaidie kuharakisha mradi wake wa hospitali anaotarajia kuijenga Bukoba.

Kwa mujibu wa Dk. Slaa, barua pepe ambazo zimekuwa zikiandikwa na Rugemalira ni kithibitisho tosha kwa kile kinachocheleweshwa maazimio yaliyofikiwa na Bunge.

“Sakata la Escrow bado ni bichi sana limeleta mgongano wa mihimili miwili, hii ni dira sahihi nchi haina maamuzi, tumeshtushwa Kikwete anamtii mtu binafsi badala ya Bunge,” alisema.

Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho bara, John Mnyika, alisema mashauri yaliyofunguliwa mahakamani, tayari Chadema imemtuma Wakili wa utetezi, Peter Kibatara, kufahamu msingi wa kesi ni upi.

Mnyika alisema baada ya chama kujiridhisha kuhusiana na msingi wa kufunguliwa mashauri hayo, sekretarieti ya chama itayajadili na kuyatolea maamuzi baadaye.

Aidha, alitoa wito kwa Rais Jakaya Kikwete kutoa mwelekeo na msimamo wake kuhusu maazimio ya Bunge yaliyofikiwa kwa sababu hakuna hukumu yoyote ya kuyafuta iliyotolewa na mahakama.

“Wamesema Kikwete atazungumza na wazee lakini wameahirisha hadi Jumatatu, hata kama yupo Arusha kule kuna wazee anaweza kuzungumza sehemu yoyote ikiwa yupo nchini, aliahidi atalitolea maamuzi suala hilo wiki moja sasa ni wiki ya pili,” alisema.

Kuhusu kauli ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, Profesa Anna Tibaijuka kuwa, akijiuzulu Rais atashangaa, Mnyika alisema Kikwete anatakiwa kueleza kama anakubaliana na hilo.

“Nina taarifa za ndani ya Ikulu kuwa, inataka kufanya uchunguzi wake, Takukuru wameshakabidhi ripoti ya pili ya nyongeza, kwa hiyo ipo sababu ya Rais kuchukua hatua, endapo hatua hazitachukuliwa tutaeleza hatua gani tutachukua,” alisema.

UCHAGUZI S/MITAA
Dk. Slaa alisema Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia wajiuzulu, kwa kusababisha uchaguzi wa serikali za mitaa kuvurugika.

Alisema licha ya wananchi kupiga kura, baadhi ya maeneo wasimamizi wa uchaguzi kwa makusudi wamegoma kutangaza matokeo na wengine wameuvuruga kwa sababu CCM imeshindwa.

Alisema wana taarifa za kubadilishwa majina ya walioshinda Ngara na Igunga.

Pia alisema ipo nyaraka ambayo mkurugenzi anamwagiza mtendaji ahakikishe CCM kinashinda.

Aidha, alisema suala la kupita bila kupingwa ni kinyume na demokrasia na haki ya msingi ya raia ya kuchagua na kupendekeza kutumike kura za ndiyo au hapana.
Kadhalika Kamati kuu ya chama hicho imezitaka mamlaka zinazohusika kuwatambua mabalozi wa Chadema katika masuala yote yanayohitaji watu wa ngazi hiyo ikiwemo utambulisho wa ukazi.

UCHAGUZI MKUU

Alisema Kamati Kuu imepokea kwa masikitiko taarifa zinazoonyesha kuwa, hadi sasa serikali kupitia Tume ya Taifa ya Uchaguzi haionekani kujipanga kufanikisha uchaguzi huo.

Alisema juzi alitembelea vituo vya jimbo la Kawe na kubaini mashine ambazo serikali ilisema kuwa ni za kisasa,  ni mbovu na tayari amewasiliana na tume.

Mkurugenzi wa Usalama Chadema, John Mrema alisema Chadema imepeleka hati ya dharura namba 2 Mahakama ya Kinondoni kupinga mshindi wa mtaa wa Kiluvya kata ya Goba, asiapishwe na mahakama itamke kuwa uchaguzi wa nafasi ya Mwenyekiti na wajumbe viti maalum ni batili.
 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post