Dar es Salaam. Kamati Kuu ya Chadema imesema tathmini yao kuhusu
uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Desemba 14, mwaka huu
imebaini kuwa ulihujumiwa.
Pia, kimewataka Waziri Mkuu Mizengo Pinda na
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia kujitathmini na kuchukua hatua za
kuwajibika kwa kujiuzulu kutokana na kushindwa kusimamia ipasavyo
uchaguzi huo.
Hayo yalisemwa jana jijini hapa na Katibu Mkuu wa
Chadema, Dk Willibrod Slaa wakati akitoa maazimio ya kikao cha siku moja
cha kamati hiyo kilichofanyika juzi kikiwa na ajenda moja ya Uchaguzi
wa Serikali za Mitaa.
“Matatizo yaliyojitokeza yameanzia kwa Pinda na
Ghasia, kwa kutoa kanuni na miongozo ambayo imefanya vyama vya upinzani
hususan wagombea wa Ukawa kuenguliwa kwa mapingamizi yaliyokuwa na lengo
la kuibeba CCM,”
“Katika maeneo ambayo upinzani ulishinda bado
matokeo yalikuwa ngumu kutangazwa na wakati mwingine damu ilimwagika,
hii yote ni mtawala kutaka kuendelea kung’ang’ania madaraka, hujuma za
aina hii hatuwezi kuendelea kuzikubali kuendelea kutokea katika nchi
inayojinasibu kuwa ya kidemokrasia,” alisema Dk Slaa.
Aliongeza: “Tunalaani vikali na kutoa onyo kali
kwa watawala kushindwa kuheshimu demokrasia ambayo Watanzania wameamua
kuitumia kupitia sanduku la kura kwa kuwapiga na kuwaua...licha ya
hujuma hizo, lakini bado tumefanya vizuri na hasa katika majimbo ya CCM
na wanayotoka mawaziri.”
Kuhusu maeneo ambayo uchaguzi umekuwa ukirudiwa
baada ya kuahirishwa kutokana na matatizo kadhaa, Dk Slaa aliwaomba
Watanzania kutumia fursa hiyo kufanya mabadiliko ya kiutawala.
“M4C (Vuguvugu la Mabadiliko) linaanza kufanya
kazi, tunawashukuru Watanzania kwa kutuunga mkono hususan vyama vya
Ukawa na waendelee katika kufanya hivyo maeneo ambayo uchaguzi unarudiwa
ili kutoa funzo kwa CCM kwamba haina hati miliki ya nchi hii.”
“Viongozi wetu waliochaguliwa ikitokea
wanatuhumiwa kwa vitendo vya rushwa kamwe chama hakitawavumilia viongozi
hao na tutachukua hatua mara moja bila kusita ikiwamo za ndani ya chama
na hata kuwashtaki mahakamani,” alisema.
Katika matokeo ambayo wameyapata ya uchaguzi huo
alisema, wamefanikiwa kuongoza mamlaka za miji na miji midogo kutoka
miwili ya Hai na Karatu hadi 30 pande zote za nchi.
Baadhi ya mamlaka hizo na majimbo katika mabano ni
Namanyere (Nkasi),Bomang’ombe,Tunduma (Mbozi Magharibi), Katoro
(Busanda), Chato (Chato), Mbalizi (Mbeya Vijijini), Sengerema
(Sengerema), Bunda (Bunda), Tarime (Tarime), Kahama (Kahama), Kyela
(Kyela), Vunjo (Vunjo) na Kayanga (Karangwe).
“Majimbo yote haya mengi ni ya CCM na ile dhana
kwamba Chadema ni chama cha ukanda mmoja sasa uchaguzi huu umedhihirisha
kwamba Chadema ni chama cha nchi nzima, kipo kila kona na hili halina
ubishi tena,” alisema Dk. Slaa.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق