CUF waitambia CCM

Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahimu Lipumba
Uongozi wa Chama Cha Wananchi (CUF) wilaya ya Kilwa mkoani hapa,  umetamba kuwa utakiachia nafasi Chama Cha Mapinduzi (CCM) kushinda katika chaguzi zijazo kwa madai kuwa kimeshindwa  kuwatumikia wananchi na kusababisha wengi wao kukithiri kwa umaskini.
Mkurugenzi wa Siasa wa CUF wa Wilaya hiyo, Deo Said Chaurembo alitoa kauli hiyo  katika mji mdogo wa Masoko wakati akizungumzia mwenendo  wa uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika hivi karibuni.

Chaurembo alisema kuwa  katika uchaguzi huo ulioshirikisha vyama vingi vya siasa, CUF kimeungwa mkono na idadi kubwa ya wananchi, hivi kuzidi kujiimarisha kadri siku zinavyosonga mbele.

Katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika mwaka 2009, CUF wilaya ya Kilwa kilishinda vijiji 12 na kwa mwaka huu vimeongezeka hadi  kufikia 42. 

 Aliwashukuru wakazi wa wilaya hiyo kwa kukiunga mkono CUF na kuongeza idadi ya vijiji, vitongoji na mitaa.

Alisema Jimbo la Kilwa Kusini lenye vijiji 36, CUF kimenyakuwa vijiji 21 kutoka sita vya mwaka 2009 na CCM kuambulia  14.

Alisema kijiji cha Migeregere, wakazi wake hawakufanya uchaguzi kufuatia wagombea wa vyama hivyo kuwekeana pingamizi.

Kwa upande wa Jimbo la Kilwa Kasikazini lenye vijiji 53, CUF kimeongeza vijiji 13 kutoka vinane vya mwaka 2009 na kufikia 21 huku CCM iking’ara kwa kujinyakulia vijiji 32.

Kwa upande wa mitaa iliyopo katika miji midogo ya Masoko na Kivinje, Chaurembo, alisema  CUF kiliigararaza CCM kwa kushinda mitaa 16 kati ya 20 na kuiachia CCM minne tu ya mji wa Masoko.

Kwa upande wake, Katibu Mwenezi wa CCM wa Chama hicho wa wilaya hiyo, Mustafa Engema, amethibitisha CUF kuwapa wakati mgumu kila chaguzi zinapofanyika kutokana na kupunguza idadi ya viti vya mitaa, vijiji na vitongoji.
SOURCE: NIPASHE

Post a Comment

أحدث أقدم