ESCROW; VIONGOZI WA DINI HAMJANILISHA NENO


Askofu Method Kilaini.
NAANDIKA mada ngumu kwa sababu inahusiana na mambo ya dini; najua wengi huogopa kufanya hivi kwa sababu za kiimani. Lakini kwa kuwa hata mitume na manabii waliulizwa na wafuasi wao juu ya utumishi; nami nina jambo la kuwauliza viongozi wa dini hapa nchini.
Hoja ya msingi ni sakata la Escrow. Sina cha kuelezea kuhusu hili kwa sababu linajulikana sana. Pengine nyongeza ni namna linavyopigiwa kelele. Jamii imekuwa na majadiliano mengi, hawa wanataka hili na wale lile, kuhusu hatua za kuwachukuliwa watuhumiwa.
Naam; waliojiuzulu, waliojiwajibisha, wanaogoma kuachia ngazi na waliowekwa kiporo wanakoleza mjadala hadi kuufikisha kwenye kuikosoa hotuba ya Rais Jakaya Kikwete iliyozungumzia sakata hilo kwamba, imejaa huruma dhidi ya wezi wa mali ya umma.
Kelele zimekuwa nyingi na sasa zimefika hadi kwenye nyumba za ibada mahali ambapo pana msingi wa Uchochezi wangu wa leo. Nimefuatilia mahubiri ya mkesha wa Sikukuu ya Krismasi yaliyotolewa na viongozi mbalimbali wa Kikristo kutoka madhehebu tofauti, sakata la Escrow limelaaniwa mno!
Pamoja na utamu wa mahubiri ya neno la Mungu kunibariki, lakini kwenye sakata la wizi wa fedha za Escrow viongozi hao wa dini hawakunilisha neno. Kwa nini? Walitoa kibanzi kwenye jicho la wengine wakaacha boriti lililoko machoni mwao.
Kuitumia madhahabu ya Bwana kuishambulia serikali, kuwalaani baadhi ya watuhumiwa, kumkosoa rais kwa kuchelewa kuchua uamuzi mgumu kwa wahusika bila kuwataja waziwazi viongozi wa dini waliojichukulia fedha za dhambi ni sawa na kutoa kibanzi na kuacha boriti.
Nilitaraji; wakati Kanisa Katoliki likikemea ufisadi wa mali za umma nchini, lingekuwa mstari wa mbele kuwalaani mapadri wake walioingiziwa fedha haramu kinyume cha utaratibu.
Nilitaraji; maaskofu kwa umoja wao, wakati wakiishambulia serikali kwa kukithiri ufisadi, ingetumia nguvu zaidi ya hiyo kuwashughulikia viongozi wa dini waliojinajisi kwa kuchukua fedha chafu na bado wanaendelea kusimama kwenye mimbari kusalisha.
Ndiyo maana nasema, viongozi wa dini hawakunilisha neno nililotamani ndani ya nafsi yangu kuhusu sakata la Escrow; hoja yangu ipo kwenye mtazamo huo.
Kama waliosikiliza hotuba ya rais walishangalia baada ya Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya makazi Anna Tibaijuka, kufutwa kazi, nami ningebarikiwa zaidi kama Askofu Methodius Kilaini (aliyechota Sh 80.9 milioni), Askofu Eusebius Nzigirwa (Sh 40.4 milioni) na Padri Alphonce Twimannye Simon (Sh 40.4 milioni), wangefuata nyayo za Tibaijuka.
Pamoja na kwamba muda wa kuwawajibisha watumishi hao wa Mungu haujaisha, lakini kama viongozi wa dini walivyokuwa na kiu ya kuona serikali inalimaliza haraka suala la Escrow hata mimi natamani nao wachukue hatua mapema za kujitoa boriti machoni mwao kabla ya kutoa kibanzi machoni mwa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanayoituhumu kwa kirefu.
Kama hilo halitoshi viongozi wa dini wawekeane mikakati ya wazi ya kihuduma kwamba, matajiri wanaotajirika kwa njia zisizoeleweka waruhusiwe kufika makanisani kuungama dhambi za ufisadi na siyo kupewa nafasi ya kuchangia huduma za Mungu kwani kanisa haliwezi kujengwa kwa fedha za wizi.
Naweka wazi mambo haya kwa sababu nimeomba neema kwa Mungu niweze kuandika makala haya kwa ujasiri kwa kuwa najua wapo baadhi ya maaskofu, mapadri na wachungaji hawaenendi sawa na neno la Mungu linavyotaka lakini hawakemewi kwa nguvu za ushirikiano kama viongozi wa dini wanavyofanya dhidi ya serikali au watu walio nje ya mfumo wa kidini, jambo ambalo naamini siyo sawa! Nachochea tu!

Post a Comment

أحدث أقدم