Haikuwa busara Rais kutumia namba ya simu ya Marekani

Serikali ya Tanzani iliwahi kutoa mwongozo wa mawasiliano yote ya wafanyakazi wa Serikali na idara zake hasa yaliyohusu baruapepe, simu na vifaa vingine vya Serikali.
Hata hivyo, agizo hili siku zote limekuwa likipuuzwa. Kwa mfano, ukisoma taarifa mbalimbali za baadhi ya taasisi nyeti za Serikali zinazokwenda kwa umma, utashangaa kukuta kuna anuani za baruapepe za Google au Yahoo.
Kama haitoshi, idara nyingine za Serikali pia zinatumia mawasiliano ya Yahoo au mengine ambayo si ya Serikali ya Tanzania. Nina wasiwasi huenda anuani hizi zinatumika hata katika nyaraka nyeti kama mikataba.
Siku za karibuni, watendaji hawahawa wa Serikali walitoa mpya kwa kutupatia Watanzania namba ya simu ya Rais Jakaya Kikwete kwa lengo la kutaka kumjulia hali alipokuwa katika matibabu nchini Marekani.
Namba iliyotolewa kwa ajili ya kutuma ujumbe wa kumtakia heri Rais ilikuwa +1-646-309-2295. Hii ni namba ya Marekani si namba ya Tanzania, kwa hiyo mtu akituma ujumbe wake unahifadhiwa kwenye hifadhi fulani huko Marekani hata kama huku nyumbani nako pia itahifadhiwa na kampuni husika.
Taarifa zinasema zaidi ya watu milioni 10 walituma ujumbe mfupi kwenye namba hiyo kwa ajili kumpa pole Rais na salamu nyingine alipokuwa hospitalini na hata baada ya kutoka.
Bila shaka wengine kwa mapenzi waliyonayo kwa Rais wao walituma ujumbe zaidi ya mara moja tangu siku namba hiyo ilipowekwa hadharani na wasaidizi wa Rais.
Kama watu milioni 10 au zaidi walituma ujumbe kwenye namba ya Marekani, ina maana kuna kampuni moja huko Marekani hivi sasa imehifadhi namba za Watanzania milioni 10 au zaidi, tena bila tabu na bila makubaliano yoyote na watu husika, yaani watumiaji wa namba hizo.
Hatuna budi kuelewa kuwa Idara ya Usalama wa Taifa ya Marekani (NSA) na shirika lao la ujasusi (CIA) ni watuhumiwa wakuu wa kudukua taarifa za mawasiliano ya watu ndani ya nchi yao wenyewe na hata nje.
Najiuliza wataalamu wetu hawakuliona hili mpaka waache mamilioni ya namba za Watanzania zikusanywe?
Kwa nini watendaji wa Ikulu walitoa namba ya nje tena Marekani ambayo ni mtuhumiwa wa udukuzi, wakati tuna kampuni ya simu yenye alama ya utaifa wetu, yaani TTCL?
Bila shaka kampuni hii ingeweza kutoa namba za simu na huduma nyingine za mawasiliano, kwa ajili ya shughuli hiyo na namba zikahifadhiwa na wao wenyewe TTCL na si mataifa mengine au kampuni nyingine ya nje.
- Mwananchi

Post a Comment

أحدث أقدم