HAKUNA HOBI YA NGONO, UGONJWA TU



MARA kadhaa utakuwa umekutana na marafiki wanaozungumza maneno mengi kuhusu ngono. Baadhi wanapozungumza, wanaonyesha wazi kutopendezwa na hali yao ya kupenda ngono kupita kiasi, lakini wengine huongea kwa kujisifu kwa vile ni mahodari wa kushiriki tendo lile.
Wanaojisifu, ndiyo hawa huja na kauli kuwa wao hobi yao ni mapenzi. Neno hili, hobi, ni la kiingereza linalomaanisha kitu ambacho mtu anakipenda. Mtu atasema hobi yake ni kusoma, mwingine michezo au muziki na kadhalika. Kila mmoja anacho akipendacho, yaani akikipata hicho, roho yake inakuwa raha burudani.
Katika siku za hivi karibuni nimeshuhudia mastaa wawili wakizungumzia ngono, ambao ni Elizabeth Michael ‘Lulu’ na Baby Madaha. Lulu alisema ngono zimekuwa zikimtesa kiasi kwamba kila mara hujikuta katika hali ya kutaka kufanya mapenzi, kitu ambacho mwenyewe anaamini ana jini mahaba.
Kwa upande wake, Baby Madaha yeye anakuja live kabisa akidai kwamba, kwake yeye, kufanya mapenzi ni hobi yake, yaani ndicho kitu anachokipenda kuliko vitu vingine vyote duniani, yaani kwake yeye, kushiriki tendo akiwa na mwenzi wake ndo faraja yake.
Wazungu wana msemo wao mmoja maarufu unaosema too much of anything is harmful, kwa tafsiri isiyo rasmi ni kwamba kitu chochote ukikizidisha, kitakupatia madhara.
Kushiriki tendo la ndoa ni kitu kinachofurahiwa na wengi, wake kwa waume, ingawa kila mmoja ana aina ya ufurahiaji wake. Wapo wanaozidisha ufanyaji wa tendo hili kutokana na sababu mbalimbali. Kuna wanaofanya hivi ili kujipatia kipato. Anakesha usiku kucha akibadilisha wanaume kwa ajili ya kipato.
Lakini wapo ambao wanapenda kushiriki tendo kwa sababu ya raha tu na siyo kingine. Kwa wote wenye aina hii ya mahitaji, wanaambiwa kuwa wana pepo la ngono!Sisemi kuhusu machangudoa, kwa sababu wote tunajua kuwa hawa wanafanya hivi ili kupata hela, nazungumza na wanawake na wanaume ambao muda wote wanawaza ngono na hata wakifanya hawaridhiki. Anatoka kuchepuka sehemu, lakini anapopanda kwenye daladala macho yake yanavutiwa na mwanamke mwingine na yupo tayari kumtongoza na kulazimisha kwenda naye muda uleule.
Ukimuona mtu wa aina hii, ni wa kumsaidia kwa sababu huo ni ugonjwa. Binadamu anao uwezo mkubwa wa kuhimili hisia za mapenzi yake. Wale waliooa au kuolewa wanaweza kuwa mashahidi wazuri wa hili. Unaweza kukuta wanandoa wanakaa hata wiki mbili bila kukutana, ingawa wanalala kitanda kimoja.
Tendo la ndoa ni kitu cha afya. Mwili hujiweka vizuri zaidi kwa ushiriki wake, lakini unapozidisha dozi, ni tatizo. Ugonjwa huu unatibika, nenda hospitali, onana na daktari bingwa wa saikolojia, atakueleza kwa nini unakuwa hivyo ulivyo na nini suluhisho la kudumu.

Post a Comment

Previous Post Next Post