MWAKA UMEISHA UMEVUNA NINI


NAAM! kama kawaida tumekutana tena kwenye kona yetu ili tujuzane machache,  tumeona  wenyewe jinsi sikukuu ya Xmas ilivyokwisha, je mwenzangu ulipata au ulipatikana. Nasikia wapo waliopombeka mpaka wakazimika, mmmh makubwa watu wengine hawanywi mpaka sikukuu.
Hivyo unakunywa mpaka unazimika unategemea nini, wenzako wakubebe eeh uwape shida kwa raha zako za kijinga, haipendezi jamani kunyweni kadri ya uwezo wenu siyo lazima kikiwa kingi basi lazima ukimalize. Kunywa na kula kwa uwezo wako.
Si unakumbuka nilikueleza nilivyomuokoa mwanamke mlafi kila kitu kwake “hamu” yaani lazima kiingie mdomoni. Sasa nisingetokea kama siyo siku ya pili kwenda kupigwa bomba ni nini, tuacheni tamaa kwa kutaka kumkomoa mtu bila kujua mfukoni kwake yupo vipi.
Matokeo yake ndiyo hayo unajidhalilisha unakunywa mpaka unazimika, ya X-mas yamepita, sasa tuulizane sisi wenyewe katika pitapita yetu ya kuchuna mabuzi, tumepata nini, je mwaka huu ulikuwa wa faida au hasara kila siku kukopwa hata pesa ya sabuni   ya kufulia nguo ya ndani huna.
Usikubali kufanya kazi kwa kujifanya ubao wa matangazo kila mwenye macho ajisomee utazeeka na ubakie shangingi mstaafu mwenye sifa ya kukopwa na kupigwa mtungo tu, huna lolote la maana!
Lazima sasa hivi tujiulize tumekwama wapi na kipi ulichokifanya kukuingizia kipato, usiwe wa kwenda kila siku hujui mwisho wa mwaka kazi yako imeingiza au imetoa.

Kama haina faida badili kazi nyingine siyo lazima upigwe na baridi na kugeuzwa shamba la mbu bila faida. Usiogope kujaribu biashara nyingine huenda ikakutoa na hiyo igeuke starehe badala ya kazi.
Narudi kwako wewe wa ndani, umeumizwa mara ngapi katika ndoa yako, umegundua kosa lako nini lililomfanya mumeo asirudi mapema au kulala nje, au kazi yako kulia tu hujui lolote, haipendezi lazima ujiulize iweje zamani alikuwa mapenzi motomoto leo hii yamepungua na kuwa penzi la mgao kama umeme.
Kama utakuwa kimya kutegemea Mungu yupo nawe hujui matatizo yako talaka hiyoo unaiita mwenyewe.
Mwaka umekwisha, umegundua udhaifu wako. Hebu muda huu mchache utumie kujiuliza hata kukaa na mwenzako na kumuuliza mpenzi hebu nieleze kosa langu.

Kwa vile ni mwisho wa mwaka kila mtu atatumia nafasi hii kuzika tofauti zake na kuingia mwaka na furaha na amani ya moyo.
Nawe uliyefanikiwa utumie mwaka huu kwa mafanikio zaidi na kurudi ulikotoka, siku zote kufika kileleni ni rahisi lakini kukaa kileleni ni kazi, ni wakati wa kuimarisha yote uliyoyafanya mpaka ukajengewa nyumba au kununuliwa gari usibweteke gari zuri  likaozea uani.
Yangu ni hayo kwa mwaka 2014 na kuwashukuru wote waliofuata, wengi wamefanikiwa na waliopuuza sasa wanajuta. Si mwingine ni mimi anti Nasra Shangingi mstaafu. Heri ya mwaka mpya.

Post a Comment

Previous Post Next Post