Dar es Salaam. Hatma iwapo mashindano ya Miss
Tanzania yataendelea au yatasitishwa kwa muda, itategemea majibu ya
tathmini iliyofanyika mwishoni mwa wiki jana yanayotarajiwa kutolewa na
Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) wiki chache zijazo.
Tathmini hiyo iliyowahusisha viongozi wa Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Basata, TGNP, wadau wa sanaa na
mashirika mbalimbali, ilibaini ukiukwaji wa kanuni na mwongozo wa
mashindano hayo kwa mwaka 2014.
Kaimu Katibu Mkuu Mtendaji wa Basata, Godfrey
Mngereza aliliambia gazeti hili kuwa, iwapo Kamati ya Miss Tanzania
ikakutwa na makosa zaidi, huenda wakapewa muda wa kujitathmini na
kujipanga upya kama ilivyokuwa kwa Miss Utalii, kwani wamevunja kanuni
za usajili.
Mngereza alisema baada ya tathmini hiyo, baraza
litarudi kwenye mwongozo wa awali wa mashindano hayo kwa utaratibu wa
baraza kisha watatoa tamko, kwa sababu Lino Agency hawawezi kupewa
kibali bila tathmini ya wadau.
“Leo ndiyo tumefanya tathmini kusema kwamba majibu
yatatoka leo au kesho ni vigumu sana, tunakaa chini tunaangalia, hiki
siyo kitu pekee ambacho tunafuatilia, hawawezi kupewa kibali kabla ya
tathmini,” alisema Mngereza.
Hatua zitachukuliwa
Hata hivyo, alisema Kamati ya Miss Tanzania
kupitia kampuni yake ya Lino Agency, imekiuka kanuni na utaratibu wa
mashindano hayo na hivyo itachukuliwa hatua.
“Tukirudi katika kanuni kuna vitu vingi sana
ambavyo wamekiuka kimojawapo ni kutetea yale ambayo yalitolewa majibu
yasiyo sahihi, kwamba kamati nzima hatimaye ikasema kwamba hiki cheti
walichotuletea ni sahihi, sasa ninajiuliza wewe unawezaje kusema cheti
ni sahihi huku hujathibitisha,” alisema na kuongeza:
“Ndicho kilichojitokeza katika tathmini, alitakiwa
kuwasiliana na mamlaka husika, kama ni mtihani kuna Necta na kama cheti
cha kuzaliwa kuna Rita, kwa hiyo wasingengoja wadau wapige kelele,
waandishi wa habari wamkalie kooni kwa kulisimamia hili ndipo
utekelezaji ufanyike,” alisema.
Mngereza aliongeza kuwa hilo ni kosa mojawapo na
mwaka huu wamekiuka sheria, kwa hiyo Wizara na Basata itatoa tamko
kuhusu mashindano hayo.
“Tutakuja na majibu ya tamko la Basata kwa niaba
ya Serikali, pia ile kauli kuwa wizara iunde kamati ya kufuatilia si
sahihi, hakuna mahali ambako kisheria wizara inaweza kuunda kamati, yeye
ndiye mwenye miongozo, hivyo anatakiwa awajibike kupitia miongozo yake,
tathmini ni sehemu ya maoni ya wadau mambo ambayo yanapaswa
kubadilika,” alisema Mngereza
إرسال تعليق