
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akitoa
hotuba mara baada ya kutunukiwa Digrii ya Heshima ya Uzamivu (PhD
Honoris Causa) katika mahafali hayo ya pili ya Taasisi hiyo jijini
Arusha mwishoni mwa wiki. (Picha na Zainul Mzige wa MOblog).

-Pia asema kuwa ubishi wa siasa hauwezi kutoa majawabu ya changamoto za maendeleo
-Asisitiza umuhimu wa internet akielezea kuwa elimu ya sayansi haipatikani kwenye magazeti
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amesema kuwa kamwe Tanzania, kama ilivyo nchi nyingine yoyote duniani,
haiwezi kuendelea kwa kutegemea mazingaombwe ama ramli bila kuwekeza
kwenye maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Aidha, Rais
Kikwete ametaka Watanzania kuacha mwenendo wa kutumia ubishi wa kisiasa
kutafuta majawabu ya changamoto za maendeleo akisisitiza kuwa majawabu
ya maendeleo yatapatikana katika maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Aidha, Rais Kikwete amewataka Watanzania kuongeza kasi yao ya matumizi ya internet
akisema kuwa mfumo huo wa habari na mawasiliano ni chimbuko kubwa la
elimu ikiwemo elimu ya sayansi kuliko kutegemea kupata elimu hiyo katika
magazeti.

Mkuu
wa Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Mohamed Gharib Bilal akimtunuku Digrii ya
Heshima ya Uzamivu (PhD Honoris Causa) katika mahafali hayo ya pili ya
Taasisi hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete mwishoni mwa wiki jijini Arusha.
Rais
Kikwete aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati alipozungumza katika
Mahafali ya Pili ya Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela
iliyoko Tengeru, Arusha, taasisi ambayo hutoa shahada za juu za uzamili
na uzamivu katika sayansi, teknolojia na tafiti za kisayansi.
Akizungumza baada ya yeye mwenyewe kuwa ametunukiwa Digrii ya Heshima ya Uzamivu (PhD Honoris Causa)
katika mahafali hayo ya pili, Rais Kikwete alielekeza sehemu kubwa ya
hotuba yake kuelezea umuhimu wa maendeleo ya sayansi na teknolojia
katika uhai na maendeleo ya Tanzania na taifa lolote duniani.

Mkuu
wa Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Mohamed Gharib Bilal akimpongeza Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete mara baada ya
kumtunuku Digrii ya Heshima ya Uzamivu (PhD Honoris Causa) katika
mahafali hayo ya pili ya Taasisi hiyo yaliyofanyika jijini Arusha
mwishoni mwa wiki.
“Somo
tunalolipata ni kwamba hakuna mazingaombwe wala njia ya mkato ya
kujipatia maendeleo ya juu. Hatuna budi kuwekeza katika kuendeleza
sayansi na teknolojia nchini, kama kweli tunataka kutoka hapa tulipo.
Hakuna ramli wala pumba za uchawi zinazoweza kuendeleza nchi yetu hata
ukiimwaga pumba hiyo katika kila njia panda ya barabara na sehemu zote
za Tanzania. Bado Tanzania haitabadilika hata inchi moja,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Hatuna
budi kuwekeza zaidi katika kufundisha wanasayansi, na katika tafiti na
ujenzi wa miundombinu ya kuwawezesha wanasayansi kufanya tafiti zao. Kwa
muda mrefu sana hili ni eneo ambalo hatukulipa uzito unaostahili.”

Pichani
juu na chini baadhi ya ndugu, jamaa na marafiki waliohudhuria Mahafali
ya Pili ya Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela iliyoko
Tengeru, Arusha.
Alisisitiza: “Tumefundisha
na kuwekeza sana katika kuwaandaa vijana wetu katika fani za sayansi ya
jamii, uongozi, siasa, sheria na biashara. Pamoja kada hizo kuwa
muhimu, lakini wanasayansi ni muhimu zaidi.”
Rais
Kikwete amesema kuwa Watanzania hawana budi kusaka elimu yenye manufaa
zaidi ya maendeleo siyo kushinda katika mambo ambayo hayana manufaa kama
vile kushinda kwenye ubishi wa kisiasa. “Watanzania kwenye
ubishi wa siasa usiseme – kila mtu fundi. Wanatumia siasa kujadili
maendeleo na kazi ni kulaumu watu wengine tu.”
Kuhusu umuhimu wa kusaka elimu, Rais amesema kuwa Watanzania wanapaswa kusaka elimu kila inapopatikana. Kwenye internet,
kwa mfano, ni mahali ambako unapata kila kitu duniani. Elimu yetu hii
ya kutafutwa kwenye magazeti haitupeleki mbali – magazeti yenyewe
yamejaa siasa tupu, nani kashinda kura zaidi kuliko mwingine nani
kashinda kidogo…”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
21 Desemba, 2014


Pichani
juu na chini ni baadhi ya wahitimu wakisikiliza hotuba ya Mh. Rais Dkt.
Jakaya Mrisho Kikwete katika mahafali ya Pili ya Taasisi ya Sayansi na
Teknolojia ya Nelson Mandela iliyoko Tengeru, Arusha.

Post a Comment