Hongera Azam kuwa wasikivu

Mabingwa wa Bara kwa mara ya kwanza Azam wanarudi nyumbani keshokutwa kwa ndege, baada ya kumaliza ziara ya Uganda ya michezo ya kirafiki kwa ajili ya maandalizi ya muendelezo wa ligi kuu ya Bara.
Aidha, ziara hiyo ilikuwa mahsusi pia kwa ajili ya kutafuta uzoefu wa kucheza Ligi ya Klabu Bingwa Afrika inayoanza mwishoni mwa mwezi ujao.

Azam, ambayo kama klabu nyingine za ligi kuu ya Bara ilitoa likizo kwa wachezaji wake kwa ajili ya kuua uchovu wa raundi saba tu za michuano hiyo, iliondoka jijini kwa basi na kikosi chake kamili na ilipanga kurudi kwa usafiri huo wa siku mbili barabarani, kwa mujibu wa taarifa ya klabu ya wiki iliyopita.

Mara baada ya taarifa hiyo, lakini hasa baada ya timu kulazimika kulala mjini Kahama ili kupunguza madhila ya kukaa kwenye basi kwa kutwa nzima, tulihoji, Nipashe, busara iliyotumiwa na uongozi kutumia usafiri huo kwa masafa marefu hayo.

Tukasema baada ya kuipokea kwa mikono miwili likizo iliyotokana na mechi saba, kama timu nyingine za ligi kuu, ungetaraji Azam iwe makini kutowachosha wachezaji wake ligi ikitarajiwa kuanza tena hivi karibuni.

Tukasema ungetaraji Azam, sasa, iwe makini kwa sababu safari ya kwenda Uganda kwa basi ni mwendo usiopungua angalau siku mbili njiani ambao kwa vyovyote ungeleta uchovu mpya kwa wachezaji hao muda mfupi baada ya klabu kuwa iliwapa mapumziko ya kuondokana na uchovu.

Tunafahamu, Nipashe, ni kwa nini Azam ililazimika kwenda kutafuta mechi za kimataifa za kirafiki nje ya nchi licha ya kwamba The Express ya Uganda ilikuwa jijini Dar es alaam siku chache kabla ya safari yake.

Tunafahamu, Nipashe, pia gharama za kusafirisha timu nzima kwa njia ya anga kati ya Dar es Salaam na Entebe ni kubwa, lakini gharama hizo za timu nzima kwa njia ya anga kati ya Dar es Salaam na Entebe ni kubwa HASA kwa klabu kama Azam ambayo moja ya vyanzo vikuu vya mapato katika biashara ya mchezo wa soka duniani -- viingilio vya uwanjani -- ni kama hakipo labda tu icheze dhidi ya Simba au Yanga kwenye ligi kuu ya Bara.

Ni mazingira ambayo yalionekana kuulazimisha uongozi makini wa Azam kupeleka timu kwa basi kule ambako The Express ilitoka kwa ajili ya mazoezi na uzoefu huo wa mechi za kimataifa muda mfupi kabla ya kuanza kwa Ligi ya Klabu Bingwa Afrika.

Lakini tukasema pia, Nipashe, hasara ambayo Azam ingepata kutokana na madhara ya usafiri wa basi wa kwenda na kurudi kutoka Kampala ingefifisha faida ambayo benchi la ufundi lilikusudia kuipata.  

Tunaamini, Nipashe, hata vipigo mfululizo ambavyo Azam ilipata katika mechi za kwanza za ziara ni matokeo ya safari ya Dar-Kampala kwa basi na ndiyo sababu, basi, tumefarijika mno kusikia kuwa sasa timu itarudi nyumbani kwa njia ambayo ni sahihi kiufundi -- ya anga.

Kurudi nyumbani kwa anga kwa Azam, wawakilishi wa nchi katika michuano mikubwa zaidi ya klabu barani, ni faraja kwetu, Nipashe, kwamba kile ambacho kilikuwa kikitupa wasiwasi wa kuifanya timu hiyo ifuate mkondo wa Simba na Yanga kwenye ligi kubwa hiyo angalau kimeshughulikiwa.

Ni lazima tuseme, Nipashe, kwamba katika klabu za nyumbani, ni Azam pekee ambayo tunaona inaweza kufika pale ambapo ndugu zetu wa Kenya waliweza kupitia kwa Gor Mahia 1987 -- kutwaa ubingwa wa Afrika. Imani hii inakuja kutokana na mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo changa na kitendo cha Azam kucheza mara mbili Kombe la Shirikisho la klabu za Afrika ambapo ukiacha mwaka huu ambapo ilitolewa katika kihunzi cha kwanza:

Ilifanya vizuri zaidi miongoni mwa timu za nchini kwa kupanda ndege tatu ilipofuzu kwa mara ya kwanza.
Ingekuwa ni jambo la ajabu, basi, kwa Azam kuanza kujifunga yenyewe goli kwa kusafirisha timu kwa njia ya barabara, hata kabla haijajua mpinzani wake katika raundi ya awali, ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika msimu ujao.
 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

أحدث أقدم