Straika wa Simba, Emmanuel Okwi.
Sweetbert Lukonge na Wilbert Molandi SOKA
la Bongo kweli balaa! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya juzi Jumamosi,
Kocha Mkuu wa Yanga, Mbrazili, Marcio Maximo kutaka kurusha makonde
uwanjani baada ya kushushiwa matusi na makomandoo wawili wa klabu hiyo.
Kisa kikubwa cha tafrani hiyo, kilitokana na kiungo wa Yanga, Haruna
Niyonzima, kubadilishana jezi na straika wa Simba, Emmanuel Okwi, hatua
ambayo iliwakera sana makomandoo wa Yanga.
Tukio hilo lililokuwa la kusikitisha na kushangaza lilitokea baada ya
kumalizika kwa mechi ya Nani Mtani Jembe 2 dhidi ya Simba baada ya
kushuhudia kikosi chake kikilala kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa,
Dar.
Baada ya mechi hiyo, Makomandoo ya Yanga walijipanga mstari katika
njia ya wachezaji na viongozi kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia
nguo uwanjani hapo, ambapo kazi yao kubwa ilikuwa ni kuwazuia waandishi
wa habari wasizungumze jambo lolote na wachezaji hao.
Makomandoo hao waliendelea kufanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa
lakini mwisho walikumbana na kizingiti kutoka kwa kiungo wa timu hiyo,
Mnyarwanda, Haruna Niyonzima ambaye anatambua vilivyo kazi yake.
Niyonzima aliwagomea makomandoo hao wasimshurutishe kama mtoto wakati
alipokuwa akizungumza na gazeti hili akitoa tathmini ya mchezo huo kama
sheria za soka zinavyoruhusu, hivyo kuwaambia hawana haki ya kumzuia
asiongee na waandishi wa habari.
Kauli hiyo ya Niyonzima iliwakera makomamdoo wawili waliokuwa
wakimshurutisha na kuonekana kupandwa na jazba na kuanza kumtolea matusi
ya nguoni Niyonzima kuhusu mama mzazi wake, jambo ambalo pia
lilimkasirisha kiungo hiyo na kutokwa na machozi.
Makomandoo hao waliofahamika kwa jina moja moja, Said na Carlos,
waliendelea kumshambulia nyota huyo kwa matusi mazito mpaka alipoingia
kwenye chumba cha kubadilishia nguo, ndipo Maximo aliposikia matusi yale
na hali halisi ilivyokuwa, akatahamaki na kutaka kumfuata Said ili
waonyeshane umwamba.
Maximo alipandwa na jazba na kukurupuka kutoka chumbani na kutaka
kwenda kupambana na makomandoo hao ambao vinywa vyao vilitawaliwa na
matusi mazito na yasiyovumilika kwa binadamu yeyote.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa benchi la ufundi wa timu hiyo
wakiongozwa na kocha msaidizi, Mbrazili, Leonardo Neiva pamoja na
daktari Juma Sufiani, walifanya kazi ya ziada kumdhibiti Maximo asitoke
nje ya chumba hicho kwenda kupambana na watu hao.
Tukio hilo pia, lilishuhudiwa live na viongozi wengine akiwemo
mwenyekiti wa kamati ya vijana, Bakili Makere pamoja na ofisa habari
wao, Baraka Kizuguto ambaye muda wote alikuwa kimya huku akitikisa
kichwa kuashiria kuhuzunishwa na nidhamu mbovu iliyoonyeshwa na watu
wao.
Hata hivyo Kizuguto hakuwa tayari kulizungumzia suala hilo lakini
kocha wa timu hiyo, Shadrack Nsajigwa, alisema kuwa kitendo hicho
kilichofanywa na makomandoo hao si cha kiungwana.
Kwa upande wake Niyonzima aliliambia Championi Jumatatu kuwa, kitendo
hicho hakijamfurahisha hata kidogo kwani kufungwa ni jambo la kawaida,
hivyo anashangaa kuona makomandoo hao wanamshambulia kwa matusi ikiwa ni
pamoja na kumzuia kuzungumza na waandishi wa habari wakati wao siyo
waliomuajiri.
Licha ya viongozi kusawazisha hali ile, Said aliendelea kumuandama
Niyonzima kwa matusi na kumwambia kuwa yeye ni mkimbizi na muda wowote
ataondolewa Yanga na hana lolote anajipendekeza tu kuwa ndani ya Yanga.
Baadaye ilikuja kubainika kuwa, kisa kikubwa cha makomandoo hao
kukasirika kupita kawaida kilitokana na Niyonzima kubadilishana jezi na
Emmanuel Okwi na kuwapongeza wachezaji wa Simba baada ya mchezo.
Akiwa na jezi aliyopewa na Okwi, Niyonzima alivamiwa na makamandoo wa
Yanga na kumhoji kwa nini alikubali kubadilishana jezi na Okwi, pia kwa
nini apeane mikono na wachezaji wa Simba baada ya mechi hiyo
kumalizika.
Makomandoo hao pia waliwavamia wachezaji ndani ya vyumba vya
kubadilishia nguo na kuanza kuwabwatukia wakidai hawajitumi, tukio
ambalo Nsajigwa ameliponda vikali akisema halijengi bali linabomoa.
إرسال تعليق