Dubai. U.A.E. Waziri Mkuu Mizengo Pinda amekatiza kwa muda,
ziara yake katika Falme za Kiarabu kwa maelezo kwamba ameitwa nyumbani
na Rais Jakaya Kikwete kwa shughuli maalumu.
Waziri Mkuu ambaye yuko katika ziara ya kutembelea
nchi za Falme za Kiarabu, ikiwa ni sehemu ya kudumisha ushirikiano na
kutafuta wawekezaji, amekatisha ziara hiyo siku mbili baada ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema kujiuzulu kutokana
na kashfa ya Escrow.
Werema alijiuzulu juzi na Rais Kikwete akaridhia
hatua hiyo, huku umma ukisubiri hatua zaidi dhidi ya mawaziri na
watendaji wa Serikali waliotajwa katika sakata hilo.
Katika barua yake ya kujiuzulu, Jaji Werema
alisema ushauri wake wa kisheria kuhusu Akaunti ya Tegeta Escrow
haukueleweka na hivyo kuchafua hali ya hewa.
Kwa mujibu wa ratiba ya ziara hiyo, leo Waziri
Mkuu alitarajiwa kufanya mazungumzo na washiriki wa maonyesho ya B2B
pamoja na kutembelea maeneo mengine lakini ziara hiyo imefutwa na badala
yake anaondoka asubuhi kurudi nyumbani.
Baadaye leo Pinda alitakiwa kwenda Doha, Qatar kwa ziara kama hiyo hadi Desemba 23.
Baada ya kukamilisha jukumu aliloitiwa, Waziri Mkuu anatarajiwa kurejea Falme za Kiarabu Jumamosi kuendelea na ziara yake.
Chadema yakerwa JK kumsifia Werema
Jana, Chadema kilielezea kusikitishwa kwake na
sifa alizotoa Rais Kikwete kwa Jaji Werema kuwa ni mwaminifu na
mwadilifu wakati amejiuzulu kutokana na kashfa ya Akaunti ya Tegeta
Escrow.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika alisema kitendo cha Rais kumsifu Jaji Werema kinawakatisha tamaa Watanzania.
“Hakupaswa kupongezwa badala yake Rais angemwambia
kwamba alikuwa kwenye taratibu za kumfukuza kazi,” alisema Mnyika na
kuongeza kuwa hata watuhumiwa wengine katika kashfa hiyo wanaposikia
Rais akimpongeza mwenzao wanaona makosa yao ni jambo la kawaida
linaloweza kupongezwa.
“Hata vyombo vya dola vitaogopa kumshtaki Werema
kwa sababu amepongezwa na Rais kwamba ni mtumishi ambaye alikuwa
mwaminifu na mwadilifu,” alisema Mnyika- Mwananchi
إرسال تعليق