Arusha. Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) limetakiwa
kutekeleza agizo la Serikali la kusimamia Msitu wa Asili wa Mlima Meru
ili kuboresha uoto wa asili, badala ya msitu huo kuendelea kuwa chini ya
Wakala Msitu Tanzania (TFS).
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili
na Mazingira, James Lembeli alitoa agizo hilo, juzi wakati kamati hiyo
ilipokuwa ikifanya hitimisho baada ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya
Arusha ulipo msitu huo.
Lembeli alisema tangu 2005, kupitia Gazeti la
Serikali, GN 280, iliagizwa msitu huo kuwa chini ya Tanapa, inashangaza
kuona wakala wa msitu nchini umekuwa ukikaidi mpango huo.
“Kuanzia sasa, tunaitaka Tanapa kusimamia msitu
huu bila kuingilia maeneo ya Chuo cha Sokoine na Chuo cha Msitu cha
Olmotonyo kwa lengo moja tu la kuendelea kuhifadhi uoto wa asili wa
msitu huu kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo,” alisema Lembeli.
Alisema kuna umuhimu kwa Serikali hasa Wizara ya
Maliasili na Utalii kuingilia kati na kutatua mgogoro huo ili
kuhakikisha Tanapa kupitia Hifadhi ya Taifa ya Arusha unautunza msitu
huo na kusitishwa mpango wa uvunaji miti.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed
Mgimwa alikubaliana na uamuzi wa Kamati ya Bunge na kusema utaratibu
utazingatiwa kwa masilahi ya Taifa.
“Tutatekeleza haya tuliyoagizwa na kamati,” alisema.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق