Kampuni zinazoajiri wasiopitia mgambo kukiona cha moto



Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Subira Mgalu.
Serikali  wilayani Muheza imesema itaanza operesheni ya kukagua kampuni binafsi za ulinzi zinazoajiri watu wasiopitia mafunzo ya mgambo.
Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Subira Mgalu, alisema hayo katika sherehe za kufunga mafunzo ya mgambo 123, yaliofanyika Ngomeni, wilayani Muheza.

Alisema operesheni hiyo ni kwa ajili ya kuangalia kama walinzi walioajiriwa wamepitia mafunzo ya mgambo na kwamba kampuni itakayokutwa imeajiri mtu asiyepitia mafunzo hayo itachukuliwa hatua.

Alisema tabia hiyo inasababisha waliopitia mafunzo hayo kukosa ajira.

Aliongeza kuwa kwa sasa ofisi ya mgambo wilaya inafanya utaratibu wa kuanzisha kampuni ya ulinzi kwa lengo la kuwaajiri vijana waliomaliza mafunzo ya mgambo.

Alisema kuwa ili kuhakikisha vijana hao wanapewa kipaumbele, amewashauri kuanzisha Saccos ya mgambo ili wapate mikopo.

Aliwataka askari hao kuanza kuwa walinzi wa misitu kwa kuwa watu wamekuwa wakivuna na kuiba mbao. Aidha aliwaahidi mtu atakayekamata mbao hizo zitataifishwa na zikiuzwa asilimia 50 watapewa askari mgambo hao ili kutunisha mfuko wao wa Saccos. Aliiomba halmashauri kutenga fungu la kuwezesha mafunzo ya mgambo ili vijana wapate moyo wa kujiunga na mafunzo hayo na kupata ajira.

Wahitimu hao katika risala yao iliyosomwa na Diksoni Mdachi, waliiomba serikali kupiga vita kampuni zinazoajiri walinzi ambao hawajapitia mafunzo ya mgambo ili kutoa nafasi za ajira kwa wale wanaomaliza mafunzo hayo. Mshauri wa mgambo wilaya ya Muheza, Lukasi  Simengwa, alisema kati ya vijana waliomaliza mafunzo hayo wamo watumishi wa serikali na viongozi wa siasa.

 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post