Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imewahukumu
kunyongwa hadi kufa washtakiwa sita katika kesi ya mauaji ya askari wa
Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wa mkoani Morogoro na mfanyakazi wa
Benki ya NMB.
Mauaji hayo ambayo yalipata umaarufu na kupewa jina la mauaji ya Ubungo Mataa yalifanyika Aprili 20,2006 jijini Dar es Salaam.
Jaji Projest Rugazia amewataja washtakiwa
waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa kuwa ni Mashaka Pastory, John Mndasha,
Martine Mndasha, Haji Kiweru, Wycliff Imbora na Rashidi Abdikadir.
Jaji Rugazia anasema aliwatia hatiani washtakiwa
hao na kuwahukumu kunyongwa hadi kufa, kufuatia ushahidi ulitolewa na
mashahidi 29 wa upande wa mashtaka pamoja na vielelezo 78
vilivyowasilishwa mahakamani hapo na ushahidi wa utetezi.
“Maungamo ya washtakiwa, ushahidi wa kitaalam na
utambuzi wa washtakiwa kutambuliwa eneo la tukio inaonesha wazi walikuwa
na nia ya kujaribu kupora takribani Sh 150 milioni mali ya benki ya NMB
zilizokuwa zikisafirishwa kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro tawi
la Wami.” Anasema Jaji Rugazia.
Anasema siku hiyo ya huzuni ya Aprili 20,2006
majambazi hao walilivamia gari hilo kwa lengo la kupora lakini bila ya
kuwa na huruma yoyote walilimiminia risasi na kuwaua D 6866 Konstebo
Abdallah Marwa na mfanyakazi wa NMB tawi la Wami Morogoro, Ernest
Manyonyi.
Walifanya tukio hilo nyakati za saa 6:30 mchana,
eneo la Ubungo Mataa jijini Dar es Salaam kwenye makutano ya barabara ya
Morogoro na Sam Nujoma.
Akiendelea kusoma hukumu hiyo, Jaji Rugazia aliwaachia huru washtakiwa Rashid Lemblisi, Philipo Mushi, Yassin Juma,
Hamisi Daud, MT 77754 Nazareth Amurike, MT 76162
Emmanuel Lameck, James Chamangwana na Hussein Idd baada ya kuwaona
hawana hatia katika kesi hiyo.
Kwa upande wa washtakiwa, Jackson Issawangu aliyekuwa mshtakiwa wa sita katika kesi hiyo na Mussa Mustafa aliyekuwa mshtakiwa wa 10 waliachiwa huru awali baada ya mahakama hiyo kuwaona kuwa hawana kesi ya kujibu.
Hadi wanaachiwa huru jana, washtakiwa hao walikuwa wamekwisha kaa rumande kwa muda wa zaidi ya miaka 8.
Kwa habari zaidi Usiache kusoma gazeti lako la Mwananchi kesho

Post a Comment