![](http://www.itv.co.tz/media/image/mabaunsa14.jpg)
Kituo
cha kupigia kura kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa, vitongoji
na vijiji cha minazi mitatu kata ya kitangiri manispaa ya ilemela leo
asubuhi kiligeuka uwanja wa masumbwi baada ya mabaunsa kadhaa wa meya wa
manispaa ya ilemela Bw. Henry matata kutwangana makonde hadharani na
wafuasi wa chama cha demokrasia na maendeleo (Chadema), huku baadhi ya
vituo vya kupigia kura wilayani humo vikikabiliwa na mapungufu ya vifaa.
ITV imefika katika kituo hicho majira ya saa 5 asubuhi na kukuta
ugomvi ukiwa umepamba moto huku baadhi ya wapiga kura wakimlalamikia
diwani wa kata hiyo Bw. Henry Matata ambaye pia ni mstahiki meya wa
manispaa ya Ilemela kuchochea vurugu hizo kwa kuwatumia mabaunsa wake
kuwashambulia kwa kipigo vijana wa Chadema.
Alipoulizwa kuhusiana na vurugu hizo, meya huyo wa manispaa ya
Ilemela Bw. Henry Matata amedai kuwa chanzo cha vurugu hizo ni kutokana
na baadhi ya wafuasi wa Chadema kuanza kuwazuia baadhi ya akinamama
kupiga kura.
Msimamizi wa uchaguzi huo, ambaye pia ni kaimu mkurugenzi mtendaji
wa halmashauri ya manispaa ya Ilemela Justin Lukaza anaeleza baadhi ya
changamoto zilizojitokeza katika zoezi hilo la uchaguzi.
Katika kituo cha kupigia kura cha jiwe kuu manispaa ya Ilemela,
hadi inatimu saa 6 mchana zoezi la upigaji kura lilikuwa katika hali ya
sintofahamu hali iliyosababisha malalamiko kutoka kwa baadhi ya wapiga
kura, huku katika kituo cha Kitangiri ‘B’ orodha ya majina ya wapiga
kura iliyokuwa imebandikwa katika ofisi ya afisa mtendaji wa kata ya
kitangiri ilikuwa imefutika.
Halmashauri ya manispaa ya Ilemela ina vituo 262 vya kupigia kura
na mitaa 172 ambayo inawaniwa na wagombea wa vyama saba vya CCM,
Chadema, CUF, TLP, UDP, ACT na ADC na habari zilizotufikia hivi punde
kutoka wilayani Sengerema zinasema kuwa uchaguzi huo katika jimbo la
Buchosa umehairishwa hadi jumamosi ijayo kufuatia kukumbwa na dosari
kadhaa, ikiwemo upungufu wa vifaa vya kupigia kura na viashiria vya
uvunjifu wa amani.
- ITV
Post a Comment