Katibu tawala wa mkoa wa Mara, Benedict Ole Kuyan.
Aidha, wanafunzi 25,964 waliofanya mtihani huo wamekosa nafasi ya kujiunga na elimu ya sekondari baada ya kutofikia alama za ufaulu, licha ya shule ya kwanza kitaifa kutoka mkoani Mara.
Katibu tawala wa mkoa wa Mara, Benedict Ole Kuyan, alisema hayo wakati akitangaza matokeo ya mtihani wa darasa la saba na matokeo ya uchaguzi wa wanafunzi waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza katika shule mbalimbali za sekondari, mwakani.
Kuyan alisema licha ya shule ya msingi ya Twiboki wilayani Serengeti kushika nafasi ya kwanza kitaifa kwa ufaulu, matokeo hayo hayakusaidia mkoa kufanya vizuri na badala yake kujikuta ukishika nafasi ya 25 kati ya mikoa 25 ya Tanzania Bara.
Alisema wanafunzi 18,385 wamechaguliwa kuingia kidato cha kwanza ikiwa ni asilimia 41.4 ya wanafunzi wote 44,349 waliohitimu elimu ya msingi mwaka huu, ukilinganisha na asilimia 38.2 ya ufaulu wa matokeo ya mwaka 2013.
Aidha wanafunzi 9,724 wameshindwa kumaliza elimu ya msingi kwa mkoa wa Mara kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za vifo, utoro, mimba na uhamisho.
Katibu tawala huyo, aliwataka wadau, wazazi, walezi na wananchi kwa ujumla kukaa chini na kusaidiana na serikali katika kulitafutia ufumbuzi wa haraka, tatizo la kushuka kwa ufaulu.
Kwa upande wake Afisa Elimu mstaafu wa mkoa wa Mara, Godon Mwita, alisikitishwa na hali ya kushuka kwa ufaulu wa wanafunzi wa shule za msingi na kuitaka serikali kupitia wadau wa elimu kupata ufumbuzi wa tatizo hilo.
Alisema mkoa huo umeporomoka kutoka kumi bora kati ya miaka ya 80 hadi mwanzoni mwa miaka 2000 na sasa kushika nafasi ya mwisho.
CHANZO:
NIPASHE
إرسال تعليق