Matukio ya elimu ya kukumbukwa 2014

Matukio kadhaa yanaufanya mwaka 2014 kuwa wenye kumbukumbu ya aina yake katika sekta ya elimu nchini. Fuatana na mwandishi kujua matukio hayo ya kielimu yaliyoteka hisia za watu wengi kwa mwaka mzima.
Mfumo mpya wa madaraja ya ufaulu waibua mjadala
Februari 22, mwaka huu, Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), limetangaza Matokeo ya Mtihani wa Taifa wa kidato cha nne wa 2013, huku ufaulu ukiongezeka kwa asilimia 15.17 kupitia mfumo mpya wa upangaji ambao ulipanua wigo wa alama na madaraja ya ufaulu.
Upangaji wa alama hizo ni A: 75-100, B+:60-74, B:50-59, C:40-49, D:30-39, E:20-29 na F:0-19. Kabla ya mabadiliko hayo, alama zilizokuwa zikitumiwa kupanga matokeo ya kidato cha nne zilikuwa ni A:80-100, B:65-79, C:50-64, D:35-49 na F: 0-34.
Hata hivyo, wadau wengi wa elimu waliokosoa mfumo huo akiwamo Profesa Kitila Mkumbo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,a aliyesema mabadiliko hayo yalilenga kuongeza ufaulu ili kuridhisha wapiga kura kupitia mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Shule 10 bora 2013 zaporomoka
Julai 17, mwaka huu shule za sekondari zilizokuwa kwenye orodha ya 10 bora katika matokeo ya kidato cha sita mwaka 2013, zimeporomoka na shule isiyo maarufu ya Igowole kutoka mkoani Iringa ilichomoza kutoka nafasi ya nane hadi ya kwanza mwaka huu.
Aliyekuwa kaimu katibu mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde alisema katika matokeo ya mwaka jana, kati ya shule 10 zilizokuwa na watahiniwa zaidi ya 30, ni shule nne pekee zimeendelea kuwamo katika kundi la shule 10 bora kitaifa mwaka huu.
Shule zilizoporomoka mwaka huu ni Marian Girls (Pwani) iliyokuwa ya sita mwaka huu wakati mwaka 2013 ilishika nafasi ya kwanza. Shule zilizotoka patupu katika orodha hiyo mwaka huu ni Mzumbe (Morogoro) iliyokuwa ya pili, Ilboru Arusha (ya nne) na Mtakatifu Mary Mazinde Juu ya Tanga (ya sita).
Wizara yaifuta EMAC
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ilisikia kilio cha muda mrefu cha wadau wa elimu kuhusu kuwapo kwa vitabu visivyo kuwa na viwango vilivyokuwa vikipewa ithibati na iliyokuwa Kamati ya Kusimamia Vifaa vya Elimu (EMAC).
Septemba mosi, wizara ikaifuta kamati hiyo na kuhamishia majukumu yake kwa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET).
- Mwananchi

Post a Comment

أحدث أقدم