Arusha. Dan Kidega (41), ndiye Spika mpya wa Bunge la Afrika
Mashariki (Eala), baada ya kupitishwa kwa kauli moja kutokana na kukosa
mshindani.
Kidega, raia wa Uganda, msomi wa shahada ya sheria
kutoka Chuo Kikuu cha Makerere Uganda, anakuwa mbunge wa nne Eala
kushikilia nafasi ya Spika wa Bunge hilo lililoanza tangu mwaka 2002.
Spika mpya anachukua wadhifa huo uliobaki wazi
baada ya aliyekuwa Spika, Dk Margaret Zziwa kuondolewa madarakani kwa
matumizi mabaya ya madaraka.
Awali, kikao cha Bunge kilichoanza Saa 9:30
alasiri jana, kilitarajiwa kuwapigia kura wabunge wawili kutoka Uganda
ili kumchagua mmoja kuwa Spika, lakini Mbunge Chris Opoka-Okumu akajitoa
kabla ya zoezi la kura kuanza.
“Kwa sababu Mheshimiwa Kidega (Dan), ndiye mgombea
pekee katika nafasi ya Spika, kikanuni anakuwa mshindi wa moja kwa moja
katika nafasi hii na kinachofuata ni zoezi la kumwapisha kuwa Spika,”
alisema Naibu Katibu wa Bunge, Alex Obatre, ambaye ndiye msimamizi wa
uchaguzi.
Awali juzi, wabunge wanne kutoka Uganda walichukua
fomu za kuwani nafasi hiyo, lakini hadi Bunge linaanza, wagombea
walisalia wawili pekee ambao ni Opoka na Kidega.
Wengine waliochukua fomu lakini wakaishia hatua za awali ni Mike Sebalu na Suzan Nakaukhi.
Kiti cha Spika wa Eala kinashikiliwa kwa kupokezana miongoni mwa wabunge wa kuchaguliwa kutoka nchi tano wanachama wa EAC.
Tanzania ndiyo ilikuwa ya kwanza kushikilia nafasi
hiyo kupitia kwa Abdulrahaman Kinana aliyefuatiwa na Abdirahin Abdi wa
Kenya, aliyepokewa na Zziwa aliyeng’olewa kwa matumizi mabaya ya
madaraka, upendeleo na kauli za kuudhi kwa wabunge na watumishi wa Eala.
Uganda ndiyo yenye zamu ya kushikilia nafasi hiyo,
ndiyo maana hata baada ya Zziwa kung’olewa, nafasi hiyo ikajazwa na
mbunge kutoka nchini humo.
- Mwananchi
- Mwananchi
Post a Comment