Mke wa Balozi kujenga kijiji cha wenye ulemavu wa ngozi

Mwenyekiti wa IPP, Dk. Reginald Mengi, akifurahia jambo na balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Ali Davutoglu, (Katikati) na mkewe, Yesim Mego Davutoglu, wakati balozi na mkewe walipomuonyesha Dk. Mengi, mchoro wa kijiji cha kisasa cha kutunza watu wenye ulemavu wa ngozi, (Albinism), kitakachojengwa barabara ya Bagamoyo hivi karibuni. Kijiji hicho kitakuwa na eneo la ukubwa wa Mita za mraba 35,000. Balozi huyo na mkewe walikuwa kwenye mazungumzo na Dk. Mengi makao makuu ya IPP, jijini Dar es Salaam jana.
Mke wa Balozi wa Uturuki nchini, Yesum Davutoglu, anatarajia kuanzisha mradi wa ujenzi wa kijiji maalumu cha watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) mwakani, kwa lengo la kupambana na vitendo vya ukatili na mauaji ya albino.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Balozi wa Uturuki nchini, Ali Davutoglu, alisema mke wake  amechukua hatua hiyo baada ya kuguswa na matukio mbalimbali ya kikatili yanayowakumba na kuathiri maisha ya watu hao.

Balozi Davutoglu, aliutambulisha mradi huo kwa Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Regnald Mengi, baada ya kumtembelea ofisini kwake ambapo pia alizungumzia mambo mbalimbali ya ushirikiano kati ya Uturuki na Tanzania.

Alisema kijiji hicho kitakachojulikana kwa jina la "Ricep Tayyip Erdogan"  kitaanza kujengwa mwakani na kitakuwa na ukubwa wa mita za mraba 35,000 nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Mke wa balozi huyo, alisema anawaona watu wa jamii ya albino kama sehemu ya familia yake, hivyo amelenga kuwaweka pamoja katika kuwalinda pamoja na kupata huduma zote ikiwamo shule, hospitali, michezo na nyumba za kuabudu bila kuwa na hofu.

“Kule Uturuki tuna jamii ya albino, lakini tunawajali na kuona ni sawa kama wengine, lakini hapa Tanzania hali ni tofauti kwani wanawindwa, wanakatwa viungo na kuuawa kama wanyama, jambo hili ni baya tunatakiwa tushirikiane kupambana,” alisema Yesim.Alisema kwa kutumia kijiji hicho atapata faraja baada ya kuona mchango wake unatambulika na kuungwa mkono na Watanzania.

Akitoa shukurani kwa niaba ya Watanzania, Dk. Mengi, alisema mradi huo utakuwa mkombozi kwa watu wenye ulemavu wa ngozi kwa sababu utaondoa hali ya vitisho, hofu na kutojiamini katika maisha yao.

Alisema matukio ya ukatili yanayoripotiwa kila siku ni aibu kwa taifa na kuporomosha sifa nzuri ya nchi iliyojijengea kwa miaka mingi.

“Wenzetu wameliona hili wameamua kutusaidia, kwa upande wetu tunatakiwa kuwaunga mkono kwani ni aibu na tabia mbovu kuona albino kama mawindo,” alisema Dk. Mengi.

 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post