Leo nahitimisha mfululizo wa makala haya. Licha ya mitandao ya
kijamii kuweza kutumika dhidi ya usalama wa Taifa, pia inaweza kulinda
usalama wake na wananchi tena kwa ufasaha zaidi.
Hata hivyo, hilo linategemea namna mitandao hiyo
itakavyotumiwa na wafanyakazi katika idara za Serikali na vyombo
vilivyopewa dhamana ya kuihakikisha nchi inakuwa na ulinzi na usalama.
Kimsingi, vyombo vya ulinzi na usalama vinapaswa
kuwa tayari wakati wote kujibu au kusema kinachotolewa dhidi yao ili
kupunguza madhara yanayoweza kutokea hasa pale vyombo hivyo
vinaposhambuliwa katika mitandao ya kijamii.
Hili la vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua
hatua mapema tunaweza kuliona kwenye vurugu kati ya wakulima na wafugaji
zilizowahi kutokea siku zilizopita na hata zinazoweza kutokea.
Tunakumbuka sote kuwa yalipotokea mauaji kati ya
wakulima na wafugaji, baadhi ya watu walisambaza picha za mauaji hayo
kwenye mitandao ya kijamii. Hili lilitokea huku Jeshi la Polisi likiwa
limekaa kimya.
Pia vurugu za wilayani Siha na propaganda ya
Wamasai kuhamishwa kutoka sehemu zao kwa ajili ya wawekezaji, taarifa
zote hizi zilisambaa mapema kwa kutumia mitandao ya kijamii.
Ukweli ni kuwa kama vyombo vyetu vitaamua kufanya
kazi kwa umakini na kwa weledi, vina uwezo mkubwa wa kudhibiti matumizi
yasiyofaa ya mitandao.
Ilivyo ni kuwa vyombo vya ulinzi na usalama
vinaweza kufanya utafiti na kukusanya taarifa nyingi zaidi kuhusu
matukio yanayoweza kutokea na kuyakabili mapema zaidi kabla ya kuleta
madhara kwa taifa.
Mathalan watumiaji wote wa mitandao ya kijamii
huacha alama wanapotumia kama ni majina, picha au hata taarifa nyingine
mbalimbali.
Taarifa hizi na nyinginezo zinaweza kukusanywa na
kutumika na vyombo hivi kushugulikia mambo mbalimbali yanayoweza
kuiathiri jamii. Hivi ndivyo tunavyoweza kuwagundua wahalifu au watu
wanaotumia vibaya mitandao dhidi ya usalama wa Taifa na wananchi kwa
jumla.
Katika nchi zilizoendelea idara za Serikali hasa
majeshi na polisi yamewekeza kwenye mitandao ya kijamii kwa kutumia
kampuni binafsi, ili ziwatengenezee programu mbalimbali zakufuatilia
taarifa za matukio na watu kwa ajili ya matumizi ya majeshi na idara zao
za usalama wa taifa .
Kama kweli tunataka kushindana na kuwa juu kwenye
uwanja huu wa taarifa na maarifa kwa kutumia mitandao ya kijamii, nchi
inatakiwa kuunda mfumo wa kitaasisi kwa ajili ya upatikanaji wa taarifa
kwanza ndani ya idara zake zenyewe na pia nje ya idara- Mwananchi
Post a Comment