Wazazi wanachangia watoto kufeli

Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita Tanzania imekuwa na rekodi nzuri ya kupanua wigo wa elimu kuanzia idadi ya wanafunzi, walimu na miundombinu.
Hata hivyo, jitihada hizi hivi sasa zinaonekana kuzorota na dalili zinaonekana katika ubora unaotia shaka wa elimu inayotolewa kwenye taasisi husika.
Matokeo ya mitihani ya kitaifa katika miaka ya hivi karibuni yanashadadia ukweli wa hali mbaya ya elimu ilivyo shuleni.
Mfano mzuri wa matokeo hayo ni yale ya kidato cha nne ya mwaka 2012, ambayo yameacha historia ya kusikitisha katika sekta ya elimu kutokana na idadi kubwa ya watahiniwa kufanya vibaya katika mitihani yao.
Katika matokeo hayo, asilimia 60 ya watahiniwa walipata daraja sifuri. Wapo watahiniwa ambao hawakuamini matokeo hayo kiasi cha wengine kufikia hatua ya kujitoa uhai. Lakini wapo waliokata rufaa ili warudie mitihani upya.
Kwa kuwa matokeo hayo yalizusha mjadala mkubwa wa kitaifa, Serikali ililazimika kuunda tume maalumu kuchunguza sababu za matokeo hayo kuwa mabaya.
Kimsingi, watu wengi wanaamini kuwa miongoni mwa sababu kubwa zilizochangia matokeo hayo ni migomo ya walimu, mazingira duni ya kufundishia, kukosekana kwa mtalaa na ukosefu wa walimu wenye sifa shuleni.
Hata hivyo, Profesa Kitila Mkumbo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anasema hoja ya mtalaa inayopigiwa kelele kila kukicha, siyo sababu ya msingi ya kufeli kwa wanafunzi.
Ni wazi kuwa masuala mengine yanayochangia ufaulu mdogo katika mitihani ni wazazi kutowajibika kusimamia maendeleo ya taaluma ya watoto wao.
Kwa mtazamo wake, mchango wa wazazi katika ufaulu wa mwanafunzi unachukua asilimia kubwa kuliko muda anaoutumia akiwa shuleni.
Wadau wa elimu wanasema hadi sasa ufuatiliaji wa wazazi ni asilimia mbili tu nchini ukilinganisha na mataifa mengine.
Jukumu la mzazi ni kuhakikisha anafahamu mwenendo wa tabia za mwanaye shuleni, lakini sasa kazi hiyo wameachiwa walimu na watendaji wengine.

Post a Comment

Previous Post Next Post