Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita Tanzania imekuwa na
rekodi nzuri ya kupanua wigo wa elimu kuanzia idadi ya wanafunzi, walimu
na miundombinu.
Hata hivyo, jitihada hizi hivi sasa zinaonekana
kuzorota na dalili zinaonekana katika ubora unaotia shaka wa elimu
inayotolewa kwenye taasisi husika.
Matokeo ya mitihani ya kitaifa katika miaka ya hivi karibuni yanashadadia ukweli wa hali mbaya ya elimu ilivyo shuleni.
Mfano mzuri wa matokeo hayo ni yale ya kidato cha
nne ya mwaka 2012, ambayo yameacha historia ya kusikitisha katika sekta
ya elimu kutokana na idadi kubwa ya watahiniwa kufanya vibaya katika
mitihani yao.
Katika matokeo hayo, asilimia 60 ya watahiniwa
walipata daraja sifuri. Wapo watahiniwa ambao hawakuamini matokeo hayo
kiasi cha wengine kufikia hatua ya kujitoa uhai. Lakini wapo waliokata
rufaa ili warudie mitihani upya.
Kwa kuwa matokeo hayo yalizusha mjadala mkubwa wa
kitaifa, Serikali ililazimika kuunda tume maalumu kuchunguza sababu za
matokeo hayo kuwa mabaya.
Kimsingi, watu wengi wanaamini kuwa miongoni mwa
sababu kubwa zilizochangia matokeo hayo ni migomo ya walimu, mazingira
duni ya kufundishia, kukosekana kwa mtalaa na ukosefu wa walimu wenye
sifa shuleni.
Hata hivyo, Profesa Kitila Mkumbo wa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam anasema hoja ya mtalaa inayopigiwa kelele kila
kukicha, siyo sababu ya msingi ya kufeli kwa wanafunzi.
Ni wazi kuwa masuala mengine yanayochangia ufaulu
mdogo katika mitihani ni wazazi kutowajibika kusimamia maendeleo ya
taaluma ya watoto wao.
Kwa mtazamo wake, mchango wa wazazi katika ufaulu wa mwanafunzi unachukua asilimia kubwa kuliko muda anaoutumia akiwa shuleni.
Wadau wa elimu wanasema hadi sasa ufuatiliaji wa wazazi ni asilimia mbili tu nchini ukilinganisha na mataifa mengine.
Jukumu la mzazi ni kuhakikisha anafahamu mwenendo
wa tabia za mwanaye shuleni, lakini sasa kazi hiyo wameachiwa walimu na
watendaji wengine.
إرسال تعليق