Zanzibar. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Zanzibar
(ZBC), Hassan Abdalla Mitawi amefikishwa mahakamani kwa kosa la matumizi
mabaya ya ofisi na ukwepaji kodi.
Mitawi alipanda kizimbani jana saa tano asubuhi
katika Mahakama ya Mkoa Vuga, mbele ya Hakimu Ali Ameir na kusomewa
mashtaka mwendesha mashtaka, Abdalla Issa Mgongo ambaye alisema
mkurugenzi huyo anakabiliwa na mashtaka mawili.
Alisema shtaka la kwanza ni kukwepa kodi kinyume
na Kifungu cha 44 (1)(e) na (2) pamoja na Kifungu cha 61 vyote vya
Sheria ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar ya mwaka 2012.
Katika kosa hilo la kwanza Mitawi na Mamy James
Matata wanadaiwa kuwa kwa nyakati tofauti mwaka huu katika Jengo la
Televisheni ya ZBC, kwa makusudi walifanya biashara ya kuuza magari bila
ya kujiandikisha kuwa walipakodi na kulipa kodi hizo kwa mamlaka
husika.
Mgongo alisema katika kosa la pili la matumizi
mabaya ya ofisi kinyume na Kifungu cha 53 na 61 vya Sheria ya Kuzuia
Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar, mshtakiwa kwa nyakati tofauti, mwaka
huu katika jengo hilo la ZBC akiwa mkurugenzi mkuu alitumia nafasi yake
kufanya biashara ya kuuza magari kwa lengo la kujipatia masilahi
binafsi.
Hakimu Ameir alimtaka mshtakiwa huyo kutojibu
lolote kwa sababu Mahakama yake haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo
hivyo hadi itakapofikishwa mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu.
Mshtakiwa yuko nje kwa dhamana ya maandishi ya Sh1 milioni pamoja na wadhamini wawili kwa kiwango hichohicho kwa kila mmoja.
- Mwananchi
- Mwananchi
Post a Comment