Mkurugenzi wa ZBC apandishwa kizimbani Zanzibar

Zanzibar. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), Hassan Abdalla Mitawi amefikishwa mahakamani kwa kosa la matumizi mabaya ya ofisi na ukwepaji kodi.
Mitawi alipanda kizimbani jana saa tano asubuhi katika Mahakama ya Mkoa Vuga, mbele ya Hakimu Ali Ameir na kusomewa mashtaka mwendesha mashtaka, Abdalla Issa Mgongo ambaye alisema mkurugenzi huyo anakabiliwa na mashtaka mawili.
Alisema shtaka la kwanza ni kukwepa kodi kinyume na Kifungu cha 44 (1)(e) na (2) pamoja na Kifungu cha 61 vyote vya Sheria ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar ya mwaka 2012.
Katika kosa hilo la kwanza Mitawi na Mamy James Matata wanadaiwa kuwa kwa nyakati tofauti mwaka huu katika Jengo la Televisheni ya ZBC, kwa makusudi walifanya biashara ya kuuza magari bila ya kujiandikisha kuwa walipakodi na kulipa kodi hizo kwa mamlaka husika.
Mgongo alisema katika kosa la pili la matumizi mabaya ya ofisi kinyume na Kifungu cha 53 na 61 vya Sheria ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar, mshtakiwa kwa nyakati tofauti, mwaka huu katika jengo hilo la ZBC akiwa mkurugenzi mkuu alitumia nafasi yake kufanya biashara ya kuuza magari kwa lengo la kujipatia masilahi binafsi.
Hakimu Ameir alimtaka mshtakiwa huyo kutojibu lolote kwa sababu Mahakama yake haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo hivyo hadi itakapofikishwa mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu.
Mshtakiwa yuko nje kwa dhamana ya maandishi ya Sh1 milioni pamoja na wadhamini wawili kwa kiwango hichohicho kwa kila mmoja.
- Mwananchi

Post a Comment

أحدث أقدم