Mshtakiwa Zuberi Lubengela (70) akiwa chini ya
ulinzi wa askari polisi baada ya kuhukumiwa kwenda jela miezi sita na
Mahakama ya Wilaya ya Kigoma kwa kosa la kukata mti wa aina ya mgunga
wenye thamani ya Sh. 100,000, mali ya kanisa la TAG kinyume cha sheria,
jana.PICHA JOCTAN NGELLY, KIGOMA
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, David Ngunyale, baada ya upande wa mashtaka kuiridhisha mahakama kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo.
Hakimu Ngunyale alisema mahakama inatoa adhabu kali dhidi ya mshtakiwa ili iwe fundisho kwake na kwa wazee wengine wenye tabia kama yake.
Alisema upande wa mashtaka ulipeleka mashahidi wawili mahakamani hapo ambao walithibitisha kuwa mshtakiwa huyo alikata mti aina ya mgunga wenye thamani ya Sh. 100,000 mali ya kanisa la TAG kinyume cha sheria.
Hakimu huyo alisema mshtakiwa alingia kwenye shamba la kanisa hilo na kukata mti huo bila idhini ya mchungaji wa kanisa hilo, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.
Alisema mshtakiwa ametiwa hatiani kwa kosa aliloshtakiwa nalo na kabla ya kutoa hukumu alimtaka ajitetee.
Mshtakiwa huyo alijitetea kuwa, ana watoto tisa wanaomtegemea, wake wawili wanaomtegemea, hivyo anaomba mahakama imhurumie na impunguzie adhabu.
Hakimu Ngunyale alitupilia mbali utetezi huo na kusema mshtakiwa atakwenda gerezani miezisita ili akajifunze namna ya kuishi na jamii na akimaliza kifungo hicho atakuwa raia mwema.
Awali, akisoma hati ya mashtaka, Inspekta wa Polisi, Athumani Mshana, alidai kuwa, Mei 9 mwaka huu, saa 3 asubuhi, katika Kijiji cha Kiganza, wilaya ya Kigoma, mshtakiwa bila halali na kwa makusudi alikata mti aina mgunga wenye thamani ya Sh. 100,000 mali ya kanisa la TAG, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.
CHANZO:
NIPASHE
إرسال تعليق