WAKAZI wa jiji la Dar
es Salaam wamelalamikia madereva wa daladala kuendelea na tabia ya
kukatisha ruti wakati wa usiku na asubuhi na kusababisha kero kwa
abiria.
Wakizungumza na Majira
jana jijini Dar es Salaam baadhi ya abiria wamewalalamikia madereva
wanaokatisha ruti na kusababisha abiria kupata usumbufu mara kwa mara.
Mmoja wa wananchi hao,
Fadhili Luweka, ambaye ni mkazi wa Gongolamboto amesema kuanzia saa
mbili usiku magari mengi yanayoelekea Gongolamboto kutoka Ubungo
yanaishia Buguruni hali inayowalazimu wakazi wa Gongolamboto kutafuta
usafiri mwingine wa kufika huko. Hali hii inawakera sana abiria kwani
inawalazimu watoe nauli mara mbili tofauti na vile ilivyopangwa na
Serikali.
"Wakati mwingine abiria
wanalipishwa nauli ya sh. 1,500 kutoka Buguruni hadi Gongolamboto
ambapo nauli halali ni sh. 400, jambo ambalo ni kinyume kabisa na nauli
iliyowekwa na Serikali," alisema Fadhili Luweka, Said Digelo, ambaye pia
ni mkazi wa Gongolamboto amelalamika kufupishwa kwa masafa, na pia
ameshauri kuwa trafiki wawepo barabarani mpaka saa tano usiku ili
kudhibiti vitendo hivyo viovu vinavofanywa na madereva wa daladala kwa
kuwa wanafupisha ruti.
"Magari mabovu
yanaingizwa barabarani kuanzia saa mbili usiku yanabeba abiria, hali
inayohatarisha maisha ya abiria kwani magari haya hayana vigezo
vinavyuruhusu kubeba abiria, na madereva wanayaingiza barabarani pale tu
wanapohakikisha trafiki wameondoka barabarani," alisema Said Digelo.
Ramadhani Mwinyimkuu
ambaye ni mkazi wa Mabibo alisema tatizo hili linamwathiri maana
inamlazimu kuchukua gari la pili au hata pikipiki ili kumfikisha
nyumbani kwake akiwa amechelewa.
Mwinyimkuu ametoa mwito
kwa uongozi wa Sumatra kuwawajibisha madereva wa daladala wanaokiuka
maadili ya kazi yao. "Ukiangalia kisheria wanapaswa kuwafikisha abiria
kwenye kituo husika lakini wanakatisha safari.
Dereva wa daladala la
Ubungo mpaka Segerea, ambaye hakutaja jina lake amekiri kufanyika kwa
vitendo hivyo. Alisema madereva wa daladala wanapunguza masafa kutokana
na tatizo la foleni, msongamano wa magari wakati wa usiku na asubuhi
unachukua muda wa saa mbili hadi tatu ili kufika kituo cha mwisho hali
inayosababisha wakatishe ruti.
"Wakati mwingine
tunalazimika kukatiza safari ili kukamilisha mahesabu ya siku husika,
kama nikiendesha gari kutoka Ubungo hadi Buguruni ninalipwa sh. 400,
kwanini niende mpaka Segerea ambapo itanichukua muda mrefu zaidi
ikilinganishwa na Buguruni ambapo nitaenda na kugeuza upesi," alisema.
Pascal Kavishe ambaye
ni dereva wa magari yanayofanya safari za Ubungo kuelekea Tegeta Nyuki
amekiri kuwepo kwa tatizo hilo.Alisema hali hiyo inasababishwa na
madereva wachache wenye uchu wa fedha ambao hawaoni tatizo kuwanyima
abiria haki yao ya kufikishwa mwisho wa kituo.
Kavishe ametoa wito kwa
chombo husika kuhakikisha kuwa shughuli za usafirishaji wa ndani ya
jiji zinaenda kama zinavyotakiwa kwa wakati wa asubuhi na usiku
- Majira
إرسال تعليق