CHADEMA yahoji pongezi za Kikwete kwa Werema

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) John Mnyika, amemtaka Rais Jakaya Kikwete, kabla ya kutoa hukumu ya Akaunti ya Tegeta Escrow atoe maelezo kuhusiana na pongezi alizozitoa kwa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Fredrick Werema baada ya kujiuzulu.

Mnyika, alitoa kauli hiyo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na Rais kumpongeza Jaji Werema kwa uamuzi wake wa kujiuzulu.

Alisema Jaji Werema alimwandikia barua ya kujiuzulu Rais Kikwete na kwamba katika majibu yake, Rais amempongeza kwa kujiuzulu kwake, huku akimpongeza kwa kazi nzuri aliyokuwa akiifanya kwa weledi alipokuwa madarakani.

“Inasikitisha sana kuona baada ya Jaji Werema kujiuzulu, Rais Kikwete anampa pongezi kufanya kazi kwa weledi kipindi alipokuwa madarakani...ni pongezi gani hizo? Hastahili kupewa mtu kama huyo ambaye ameiingizia hasara serikali ya mabilioni ya fedha kupitia akaunti Escrow,” alisema Mnyika.

Alimtaka Rais Kikwete atoe tamko kuhusiana na wengine waliobaki ambao walihusika katika sakata hilo kama atawawajibisha pamoja na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.

- Majira

Post a Comment

أحدث أقدم