Siha. Serikali imetangaza kuanza msako wa
kuwatafuta viongozi wa kisiasa na watu wengine, waliopanga na kuratibu
tukio la kuchoma moto Kambi ya Watalii ya Ndarakwai wilayani Siha.
Kambi hiyo yenye hoteli ya kitalii yenye hadhi ya
nyota nne na shamba kubwa lenye wanyama wa kila aina isipokuwa simba,
inamilikiwa na mwekezaji Peter Jones ambaye ni raia wa Uingereza.
Katika tukio hilo lililotokea Novemba 14 mwaka
huu, nyumba 16, magari 11 na mali nyingine, zote zikiwa na thamani ya
Sh1.5 bilioni, ziliteketezwa kwa moto huo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa
Wilaya ya Siha, Dk Charles Mlingwa alisema kazi kubwa inayofanyika sasa
ni kukusanya taarifa za kiitelijensia za vinara waliopanga tukio hilo.
“Tunaendelea na kazi kubwa ya kutambua waliopanga
na kusimamia uharibifu wa mali kwa sababu sisi kama Serikali tunaamini
lazima jambo hili lilipangwa na watu,” alisema mkuu huyo wa wilaya.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya, shamba hilo
lipo Wilaya ya Siha na sio Longido kama ambavyo baadhi ya wananchi wa
jamii ya wafugaji wa Kabila la Wamasai wanavyodai ili kuhalisha uhalifu
huo.
“Madai ya kuliunganisha suala hili la kihalifu na
masuala ya kimipaka ni njia tu ya mtu kujaribu kuficha uhalifu wake.
Hili si suala la mipaka, hili ni suala la kihalifu,” alisisitiza mkuu
huyo wa wilaya.
Dk Mlingwa alisema amekuwa DC wa wilaya hiyo kwa
miaka mitatu mfululizo na hakuna kikao hata kimoja cha kiserikali wala
cha kijamii kilichowahi kuletewa taarifa za kuwapo mgogoro wa kimipaka.
Alisema Serikali itatumia vyombo vyake kuhakikisha
ulinzi na usalama unakuwepo kwa wananchi wa wilaya hiyo, wawekezaji na
watalii wanaopanda mlima kupitia lango la Londorosi.
“Nataka niwahakikishie watalii kuwa Siha ni
salama. Tunaomba radhi kwa kilichotokea kwa sababu tunawajibu wa kuzuia
uhalifu lakini wakati mwingine mhalifu anakuja na mbinu tofauti,”
alisema.
Kwa upande wake, Jones alisema tukio hilo
limewasababishia hasara kubwa ikiwamo kupoteza biashara ya zaidi ya
Sh210 milioni kwa watalii ambao wangelala hotelini kwao kati ya Novemba
na Machi 2015.
“Siku ile ya tukio tulikuwa na bookings nyingi
sana mwisho wa mwezi wa 11 na 12. Tulikosa biashara ya karibu Sh60
milioni ya wageni ambao walikuwa walale kwetu miezi hiyo miwili,”
alisema Jones.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق