Mtendaji wa kijiji avamiwa, ajeruhiwa

Afisa Mtendaji wa kijiji cha Mbambara, Kata ya Kwafungo, wilayani Muheza, Tanga,  Lusian Mbawala, amejeruhiwa vibaya kichwani na watu ambao hawajafahamika.
Tukio hilo lilitokea juzi eneo la njia panda ya kwenda kijiji cha Kirongo baada ya kukutana na watu hao usiku wakiwa na silaha za jadi.

Afisa mtendaji huyo ambaye amelazwa katika hospitali Teule wilaya ya Muheza, alimweleza mkuu wa wilaya ya Muheza, Subira Mgalu, ambaye alifika hospitalini hapo kumjulia hali kwamba alipigwa na watu  ambao hakuwatambua.

Mtendaji huyo ambaye wakati anashambuliwa alikuwa akiendesha pikipiki, alisema alipofika maeneo ya njia panda ya kwenda kijiji cha Kirongo walijitokeza watu hao na kumpiga na kitu kizito kichwani.

Alisema kuwa baada ya kuona hali hiyo alitelekeza pikipiki na kukimbia porini kwa miguu ili kukwepa asipoteze maisha.

Alisema kuwa alijikongoja huku damu ikiwa inavuja mpaka katika nyumba za watu kisha akatoa taarifa ndipo watu walitoka na kuelekea sehemu ya tukio na kuikuta  pikipiki, lakini walishakimbia.

Alisema kuwa katika tukio hilo watu hao walimuibia simu ya mkononi na fedha  taslimu Sh. 60,000.

Mkuu wa wilaya ya Muheza, Subira Mgalu, alisema kuwa atawasiliana na kamanda wa polisi wilaya ya Muheza kuhusu hilo ili hatua zichukuliwe haraka

Diwani wa kata ya Kwafungo, Gabriel Mswagala na Mwenyekiti wa kijiji cha Mbambara, Teddy Fidelisi, kwa nyakati tofauti walisema tukio hilo limehusisha na masuala ya kisiasa katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post