Waziri Masele aporwa na vibaka

Naibu Waziri wa Nishati na Madini,Steven Masele.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Steven Masele, ambaye pia ni Mbunge wa Shinyanga Mjini, amevamiwa na kundi la vibaka wakati akielekea zahanati kupatiwa matibabu na kisha kuporwa vitu mbalimbali mjini Shinyanga.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Masele alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 4:00 usiku, wakati akienda kupatiwa matibabu ya matatizo ya koo katika zahanati ya Bakwata, ghafla alivamiwa na kundi la vijana wapatao 30 na kumpora mali zake.

Masele alisema akiwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, wakipata chakula cha usiku hotelini mjini hapa, ghafla alijisikia vibaya hivyo kuamua kwenda kupata matibabu katika zahanati ya Bakwata ambako akiwa njiani alikumbana na mkasa huo.

“Wakati nafika katika zahanati hiyo, ghafla likatokea kundi la vijana zaidi ya 30 na kuniteka, wakanipora simu yangu aina ya Galaxy yenye thamani ya Sh. milioni moja, fedha taslimu Sh.50,000 pamoja na kadi za benki,” alisema Masele.

Masele alikanusha tuhuma alizozushiwa kuwa kuporwa huko kulitokana na kugawa rushwa kwa wananchi wakati wa kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa, ili wananchi wawachague wagombea wa CCM.

Aidha, alitumia fursa hiyo kuwatoa hofu wapiga kura wake kuwa vibaka hao hawakumdhuru na hali yake ni nzuri, isipokuwa walichukua vitu hivyo na kukimbia baada ya polisi kufika eneo la tukio na kufyatua risasi hewani.

Kamanda wa Polisi Mkoani Shinyanga, Justus Kamugisha, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa baadhi ya vibaka hao wamekamatwa jeshi lake linaendelea na upelelezi wa kuwabaini wengine waliohusika.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post