Marehemu Alfred Ghozi enzi za uhai wake.
HUZUNI,
vilio, majonzi vilitawala kwa wakazi wa Kiabakari na vitongoji vyake
kufuatia Mwalimu Alfred Ghozi (26) (pichani) wa Shule ya Sekondari ya
Kukirango iliyopo Kata ya Kukirango, Halmashauri ya Butiama mkoani Mara
kukutwa amechinjwa kama kuku kwa kutumia panga.
Mama wa marehemu Alfred Ghozi (26) akihuzunika kumpoteza mwanaye.
Tukio
hilo la kutisha lilijiri mwanzoni mwa mwezi huu, katika Kitongoji cha
Kyawazaru Kata ya Kukirango wilayani Butiama, Mara.Licha ya kuchinjwa
shingo, mwili wa marehemu huyo ulikutwa na majeraha kibao ikiwemo tumbo
lake kupasuliwa na macho kutobolewa kwa kitu chenye ncha kali.
WACHINJAJI AKINA NANI?
Chanzo
cha habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara zinasema,
mwalimu huyo alichinjwa kikatili na watu wasiojulikana lakini awali
alipigiwa simu na mwanafunzi wake mmoja wa kidato cha nne (jina
tunalihifadhi kwa sasa), mwenye umri wa miaka 23 ambaye alitoweka na
anatafutwa.
DAKIKA ZA MWISHO ZA UHAI WAKE
Taarifa
zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, ACP Alex
Kalangi zinaelezea kwa kina jinsi mwalimu huyo alivyopita katika dakika
za mwisho za uhai wake wa duniani.
Waombolezaji wakimfariji mama wa marehemu Alfred Ghozi msibani.
Inadaiwa
Desemba 7, mwaka huu, saa 1:30, marehemu aliondoka Kiabakari akiaga kwa
watu wake wa karibu kwamba anakwenda kwenye Mgodi wa Dhahabu wa Kataryo
uliopo kata hiyo baada ya kupigiwa simu na mwanafunzi huyo aliyekuwa
akimdai shilingi 450,000.
“Kwa
mujibu wa vyanzo vyetu ni kwamba mwanafunzi huyo alimpigia simu mwalimu
wake aende mgodini ili akamlipe fedha alizokuwa akimdai.“Mwalimu huyo
kwa vile alikuwa na safari ya kwenda kwao, Kagera kwa likizo ya Desemba
aliamua kuzifuata fedha hizo kama alivyaombiwa na mwanafunzi wake,”
kilisema chanzo ndani ya jeshi la polisi.
MWALIMU AENDA KIMOJA
Habari
zaidi zinasema, mara baada ya Mwalimu Ghozi kwenda kuitikia wito wa
mwanafunzi wake ambaye pia anajishughulisha na uchimbaji wa dhahabu
kipindi hiki cha likizo, hakurejea tena nyumbani kwake.
Ilipofika
Desemba 9, mwaka huu, baadhi ya watu wake wa karibu walianza kujiuliza
kisa cha mwalimu huyo kutorejea kwake lakini halikupatikana jibu la
wazi.
Ndugu na jamaa wa karibu wakitoa heshima zao za mwisho kwa marehemu Alfred Ghozi.
Wapo
waliokataa kuamini kwamba huenda alikutana na mkasa mzito njiani
akienda au akirejea kwa vile mwalimu huyo hakuwa na tabia ya kumuwezesha
kuwa na maadui.
WANANCHI WAKUSANYIKA
Baada
ya kuona hali si ya kawaida, baadhi ya wananchi, wakiwemo bodaboda wa
Kiabakari, walikusanyika wakiongozwa na wapanda pikipiki wa Kiabakari na
kuelekea mgodini ambako mwalimu huyo aliaga anakwenda kufuata fedha
zake.
Lakini
wakiwa wanakaribia mgodini, walimkuta mwalimu huyo kichakani akiwa
umechinjwa shingo, mwili wake umekatwakatwa sehemu mbalimbali hasa
tumboni kiasi cha kuufanya utumbo kuwa nje.
MWANAFUNZI ATOROKA
Akiongoza
waombolezaji katika shughuli ya kuuaga mwili wa mwalimu huyo, Desemba
10, mwaka huu katika Viwanja vya Shule Sekondari ya Kukirango, Mkuu wa
Wilaya ya Bitiama, Angela Mabula alilaani mauaji hayo ya kinyama.
Mabula
akawataka wananchi kushirikiana na polisi kuwajua watu waliomchinja
mwalimu huyo, akiwemo mwanafunzi huyo ambaye inaaminika alitumika
kumuita marehemu kwa kumlaghai kuwa anataka kumlipa deni lake kumbe
sivyo.
“Wahusika
wote wa mauaji hayo akiwemo mwanafunzi wametoroka, hivyo kuwapa kazi
polisi kuwasaka na kuwakamata ili wawafikishe kwenye vyombo vya sheria,
mshirikiane nao,” alisema mkuu huyo wa wilaya.
Kamanda
Kalangi aliyekiri kutokea tukio hilo, alisema hajakamatwa mtu yeyote
kuhusiana na mauaji hayo lakini makachero wa polisi bado wapo kazini
wakiendelea na msako.
Marehemu alizikwa Mjini Bukoba, Kagera mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amina.
CHANZO: UWAZI/GPL
إرسال تعليق