Nassari kizimbani, adaiwa kuchoma bendera ya CCM


Arumeru/Songea/Pwani. Mamia ya wakazi wa Jimbo la Arumeru Mashariki, jana walifurika katika Mahakama ya Mwanzo ya Maji ya Chai kusikiliza kesi inayomkabili Mbunge wa jimbo hilo, Joshua Nassari ya kuchoma bendera ya CCM yenye thamani ya Sh250,000.
Nassari alifikishwa katika mahakama hiyo saa tano asubuhi akitokea rumande ya Kituo cha Polisi Usa River ambako alilala baada ya kukamatwa juzi jioni.
Mbunge huyo alipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo, David Mwita kuwa alichana na kuichoma bendera hiyo juzi saa 11 jioni katika eneo la Maji ya Chai.
Ilielezwa kuwa mbunge huyo akijua anavunja sheria, kifungu cha 326 cha makosa ya jinai, alichoma bendera hiyo mali ya Raphael Moses.
Mbunge huyo kwa tiketi ya Chadema alikana mashtaka hayo na aliachiwa kwa dhamana hadi Desemba 24.
Wakati kesi hiyo ikiendelea, mawakili watatu walifika kumtetea lakini hawakupewa nafasi ya kuzungumza kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kutumia mawakili.
Nje ya Mahakama
Baada ya Nassari kutoka nje akiwa ameambata na Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema alibebwa juujuu na wafuasi wa chama hicho huku wakiimba Mandela! Mandela! Mandela!
Akizungumza na wafuasi hao, alisema kesi hiyo ni ya kisiasa na inatokana na hasira za Serikali ya CCM kushindwa vibaya katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika jimbo hilo.
Wafuasi CUF mbaroni
Wafuasi wanne wa CUF katika Mamlaka ya mji mdogo wa Utete, Rufiji, wamekamatwa na polisi kwa tuhuma za kuvunja vioo katika jengo la ofisi ya CCM Wilaya ya Rufiji na ofisi mbalimbali za Serikali wakidai wamehujumiwa katika uchaguzi huo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei aliwataja wanaoshikiliwa na polisi kuwa ni Issa Ngosho, Jumanne Ngosho na mtu mmoja aliyetajwa kwa jina moja la Rwambo na mkewe ambao walikamatwa juzi jioni majumbani mwao.
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post