Ndoa za mkeka zasababisha kuongezeka kwa talaka

TAMWA.
Kukithiri  kwa ndoa za mikeka imesababisha kuongezeka kwa idadi ya kesi za talaka katika mahakama za Zanzibar.
Akizungumza mjini Zanzibar hivi karibuni, Mwanaharakati kutoka chama cha wanahabari wananake nchini (Tamwa) Amina Talib Ali, alisema ndoa hizo maarufu kama `ndoa za kukamatiwa’ zinaharibu mfumo mzima wa maisha ya vijana.

Alisema kwa mujibu wa ripoti zilizotolewa na Tamwa, Mahakama za kadhi zenye jukumu la kusikiliza kesi za ndoa na mirathi, zimeelemewa na idadi kubwa ya maombi ya talaka na kupelekea watendaji wake kulalamikia wananchi kwa kutochukua hatua.

 “Mtindo huu wa ndoa za kukamatiwa umekuwa wa kawaida ukiendelezwa hapa kwetu Zanzibar, unasababisha vijana wengi kushindwa kutunza familia zao baada ya kukosa uwezo, matokeo yake kuna ongezeko kubwa la kesi za talaka na watoto wanaohitaji misaada,” alisema Amina.

Aliwataka wazazi kuchukua jukumu la kuwalea watoto katika maadili ili kukwepa vitendo vya ushawishi wa kuingia katika mahusiano ya kimapenzi kabla ya umri wao.

Hata hivyo, aliishauri serikali kuangalia namna ya kuboresha sheria ambayo itaweza kuzuia wazazi kuchukua jukumu la kuwaozesha watoto wao mapema kabla hawajapevuka kiakili na kimaamuzi.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

أحدث أقدم