NEC kusimamia uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa

Dar es Salaam. Kilio cha wadau wa uchaguzi kimesikika hatimaye, baada ya Serikali kutangaza nia yake ya kuufanya uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2019 kusimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Hayo yalielezwa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia kuwa hata mwaka huu, Serikali ilikuwa imeomba NEC iusimamie lakini ikashindikana kutokana na tume hiyo kutingwa na shughuli nyingi.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa NEC, Julius Malaba alishindwa kukubali wala kukataa kuhusu kuwapo kwa mpango huo alipoulizwa jana, badala yake alisema atafutwe leo kwa ufafanuzi zaidi. “NEC walikubali, lakini pia walitueleza ugumu wa jambo hili kwa sasa. Ni kuhusu Daftari la Kudumu la Wapigakura wanalolitumia katika Uchaguzi Mkuu, walisema ni ngumu kutumia daftari hilo katika uchaguzi wa Serikali ya Mtaa,” alisema Ghasia.
Kwa muda mrefu, watu wa kada mbalimbali nchini wamekuwa wakishinikiza Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kusimamiwa NEC badala ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo inaongozwa na wanasiasa wenye masilahi na uchaguzi huo.
Hoja za wadau hao hazina tofauti na kasoro nyingi za uchaguzi wa mwaka huu ambao umeahirishwa katika baadhi ya maeneo na kugubikwa na vurugu za kutokuaminiana.
Hata hivyo, Ghasia alisema pamoja na kasoro hizo, mwaka huu kulikuwa na mafanikio makubwa kulinganisha na uliopita... “Mwaka 2009 mpigakura alikuwa akipewa karatasi nyeupe na kutakiwa kuandika majina ya wagombea anaotaka kuwapigia kura, ndiyo maana hakukuwa na lawama za kukosekana kwa karatasi za kupiga kura.”
- mWANANCHI

Post a Comment

أحدث أقدم