Rais aongeza miezi sita kukamilisha maabara


·        . Awapongeza wananchi na viongozi kwa kazi kubwa ya ujenzi
·        . Atunukiwa Digrii ya Heshima ya Uzamivu
·        . Achangia Sh.milioni 200 Taasisi ya Sayansi na Teknologia ya Nelson Mandela
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewaongezea muda wa miezi sita viongozi na wasimamizi wa ujenzi wa maabara katika shule za sekondari nchini, ili kuwawezesha kukamilisha kazi hiyo ipasavyo.
Aidha, Rais Kikwete ametoa pongezi kwa wananchi wa Tanzania na viongozi kwa kazi kubwa waliyoifanya katika ujenzi wa maabara nchini.
Rais kikwete pia ametangaza kuwa anachangia Sh.Milioni 200 katika Mfuko Maalum wa Dhamana (Endowment Fund For Excellence) wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (The Nelson Mandela African Institution of Science and Techonolgy).
Rais Kikwete ametangaza mambo hayo makubwa jana, Alhamisi, Desemba 18, 2014, wakati alipozungumza na uongozi, wahitimu na wana-Jumuiya ya Taasisi hiyo, baada ya kuwa ametunukiwa Shahada ya Uzamivu ya Heshima (PhD honoris causa) ya taasisi hiyo katika Mahafali ya Pili ya Taasisi hiyo yaliyofanyika kwenye Taasisi hiyo Tengeru, Arusha.
Rais Kikwete alitunukiwa digrii hiyo ya heshima ya Uzamivu na Mkuu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Mheshimiwa Mohamed Gharib Bilal ambaye ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Taasisi hiyo ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela ni chombo cha aina ya pekee cha elimu ambacho hutoa wahitimu wa Shahada za Uzamili (Masters Degree) na Uzamivu (PhD) tu katika sayansi na teknolojia na ni moja ya taasisi mbili tu za aina hiyo katika Bara la Afrika.
Katika hotuba yake iliyofafanua kwa undani kabisa maana ya maendeleo ya sayansi na teknolojia katika maendeleo ya Tanzania na nchi yoyote dunia, Rais Kikwete pia alizungumzia maendeleo ya ujenzi wa maabara ya masomo ya sayansi nchini ambao lengo lake ni kutekeleza agizo lake la kuhakikisha shule zote za sekondari nchini zinajenga maabara ya kufundishia masomo ya sayansi.
Rais Kikwete alitoa agizo hilo miaka miwili iliyopita, Novemba 2012 na akatoa miaka miwili kukamilisha kazi hiyo ifikapo Novemba 30, mwaka huu, 2014. Rais Kikwete alitoa agizo hilo baada ya kubaini kuwa ukosefu wa maabara kwa ajili ya masomo ya fikizia, kemia na biolojia ilikuwa moja ya sababu ya kuwakatisha tamaa wanafunzi nchini kupenda masomo ya sayansi.
Aidha, Rais Kikwete alisema kuwa umuhimu wa kujenga maabara uliongezwa kasi na ongezeko kubwa la shule za sekondari ambazo ziliongezeka kutoka shule 828 mwaka 2004 hadi kufikia 3, 551 kwa sasa. Kati ya shule hizo 3,551 ni shule 88 zilizokuwa na vyumba vitatu kwa ajili ya masomo hayo matatu ya sayansi.
Rais Kikwete amesema kuwa tathmini ya sasa inaonyesha kuwa zinatakiwa zijengwe maabara kwenye shule 3,463 ambazo ni sawa na vyumba 10,389 na kuwa tathmini hiyo inaonyesha kuwa hadi Desemba 7, 2014, vilikuwa vimejengwa vyumba 3,867 vya maabara ambavyo ni sawa na asilimia 37.2 ya mahitaji ambavyo vimekamilika, vyumba 5,891, sawa na asilimia 56.7 ambavyo viko katika hatua mbali mbali za kukamilishwa na vyumba 631 ama sawa na asilimia 6.1 ambavyo ujenzi wake haujaanza.
Aliongeza Rais: “Natoa pongezi za dhati kwa viongozi na wananchi wa Tanzania kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya.  Kwa ajili ya kumaliza palipoishia nawaongezea miezi sita.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
19 Desemba, 2014

Post a Comment

Previous Post Next Post