· .
Awapongeza wananchi na viongozi kwa kazi kubwa ya
ujenzi
· .
Atunukiwa Digrii ya Heshima ya Uzamivu
· .
Achangia Sh.milioni 200 Taasisi ya Sayansi na
Teknologia ya Nelson Mandela
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewaongezea
muda wa miezi sita viongozi na wasimamizi wa ujenzi wa maabara katika shule za
sekondari nchini, ili kuwawezesha kukamilisha kazi hiyo ipasavyo.
Aidha,
Rais Kikwete ametoa pongezi kwa wananchi wa Tanzania na viongozi kwa kazi kubwa
waliyoifanya katika ujenzi wa maabara nchini.
Rais
kikwete pia ametangaza kuwa anachangia Sh.Milioni 200 katika Mfuko Maalum wa
Dhamana (Endowment Fund For Excellence) wa Taasisi ya Sayansi na
Teknolojia ya Nelson Mandela (The Nelson
Mandela African Institution of Science and Techonolgy).
Rais
Kikwete ametangaza mambo hayo makubwa jana, Alhamisi, Desemba 18, 2014, wakati
alipozungumza na uongozi, wahitimu na wana-Jumuiya ya Taasisi hiyo, baada ya
kuwa ametunukiwa Shahada ya Uzamivu ya Heshima (PhD honoris causa) ya taasisi hiyo katika Mahafali ya Pili ya
Taasisi hiyo yaliyofanyika kwenye Taasisi hiyo Tengeru, Arusha.
Rais
Kikwete alitunukiwa digrii hiyo ya heshima ya Uzamivu na Mkuu wa Taasisi ya
Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Mheshimiwa Mohamed Gharib Bilal ambaye
ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Taasisi
hiyo ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela ni chombo cha aina ya pekee cha
elimu ambacho hutoa wahitimu wa Shahada za Uzamili (Masters Degree) na Uzamivu (PhD)
tu katika sayansi na teknolojia na ni moja ya taasisi mbili tu za aina hiyo
katika Bara la Afrika.
Katika
hotuba yake iliyofafanua kwa undani kabisa maana ya maendeleo ya sayansi na
teknolojia katika maendeleo ya Tanzania na nchi yoyote dunia, Rais Kikwete pia
alizungumzia maendeleo ya ujenzi wa maabara ya masomo ya sayansi nchini ambao
lengo lake ni kutekeleza agizo lake la kuhakikisha shule zote za sekondari
nchini zinajenga maabara ya kufundishia masomo ya sayansi.
Rais
Kikwete alitoa agizo hilo miaka miwili iliyopita, Novemba 2012 na akatoa miaka
miwili kukamilisha kazi hiyo ifikapo Novemba 30, mwaka huu, 2014. Rais Kikwete
alitoa agizo hilo baada ya kubaini kuwa ukosefu wa maabara kwa ajili ya masomo
ya fikizia, kemia na biolojia ilikuwa moja ya sababu ya kuwakatisha tamaa
wanafunzi nchini kupenda masomo ya sayansi.
Aidha,
Rais Kikwete alisema kuwa umuhimu wa kujenga maabara uliongezwa kasi na
ongezeko kubwa la shule za sekondari ambazo ziliongezeka kutoka shule 828 mwaka
2004 hadi kufikia 3, 551 kwa sasa. Kati ya shule hizo 3,551 ni shule 88
zilizokuwa na vyumba vitatu kwa ajili ya masomo hayo matatu ya sayansi.
Rais
Kikwete amesema kuwa tathmini ya sasa inaonyesha kuwa zinatakiwa zijengwe
maabara kwenye shule 3,463 ambazo ni sawa na vyumba 10,389 na kuwa tathmini
hiyo inaonyesha kuwa hadi Desemba 7, 2014, vilikuwa vimejengwa vyumba 3,867 vya
maabara ambavyo ni sawa na asilimia 37.2 ya mahitaji ambavyo vimekamilika,
vyumba 5,891, sawa na asilimia 56.7 ambavyo viko katika hatua mbali mbali za kukamilishwa
na vyumba 631 ama sawa na asilimia 6.1 ambavyo ujenzi wake haujaanza.
Aliongeza
Rais: “Natoa pongezi za dhati kwa viongozi na wananchi wa Tanzania kwa kazi
kubwa na nzuri waliyofanya. Kwa ajili ya
kumaliza palipoishia nawaongezea miezi sita.”
Imetolewa na:
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar
es Salaam.
19 Desemba, 2014
إرسال تعليق