Ripoti ya Tawla yabaini kukithiri kwa ukatili wa kijinsia

Dar es Salaam. Chama cha Wanasheria Wanawake (Tawla) kimezindua Ripoti ya Mapitio ya Ukatili wa Kijinsia nchini na kubaini kukithiri kwa matukio hayo waliyodai yanasababishwa na udhaifu wa sheria.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo jijini hapa jana, mwenyekiti wa Tawla, Aisha Bade alisema chama hicho kilifanya utafiti katika baadhi ya mikoa na wilaya nchini na kubaini kuwa kuna upungufu mkubwa wa kisheria katika masuala ya unyanyasaji wa kijinsia.
“Tulienda mbali zaidi na kuangalia ni kwa kiwango gani sheria na sera zinaangalia ukatili wa kijinsia,” alisema Bade.
Kadhalika Bade alisema ripoti yao ilibaini kuwa masuala mengi ya ukatili wa kijinsia yana mizizi katika usawa na yanasababishwa na wanajamii wenyewe, tamaduni na mazingira. Ongezeko la matukio ya ukatili wa kijinsia lilionyeshwa katika utafiti uliofanywa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) mwaka 2013 pekee kesi 190 za ubakaji ziliripotiwa kwenye mikoa ya Singida na Dodoma, pamoja na wilaya za Babati, Newala na Mbulu huku kesi 996 zikiripotiwa Unguja.
Kuhusu sheria zenye upungufu, Bade alisema sheria mpya ya ndoa bado haiweki wazi umri sahihi wa kuolewa, jambo linalosababisha ndoa za utotoni.
Sheria zenye udhaifu zilizoibuliwa na Tawla ni pamoja na sheria mpya ya mtoto ya mwaka 2009 ambayo haiweki wazi umri wa kuolewa au kuoa na sheria maalumu ya makosa ya kujamiiiana (Sospa).

Post a Comment

Previous Post Next Post